MRITHI wa mali ya Kampuni ya Keroche Breweries nchini Kenya, Anerlisa Muigai amefichua kuwa mpenzi wake, mwana-muziki, Ben Pol, anataka ahamie Tanzania ili kuiimarisha ndoa yake isije kuota mbawa kutokana na umbali.

Katika ujumbe wake wa Instagram, mwanzilishi huyo wa Kampuni ya Nero amedokeza hayo ila bado anaonyesha shaka kuhusu suala hilo.
Labda, kusita kwake kunatokana na kampuni yake kuwa Kenya na biashara zake nyingine nyingi.

“Mpenzi wangu amekuwa akijaribu kunisawishi siku nzima nihamie Tanzania kabisa kabisa lakini sijui kama hilo linawezekana,” aliandika Anerlisa.

Hapo awali, Ben Pol alifichua kuwa, pete aliyomvalisha Anerlisa ilimgharimu kiasi cha KSh 1.1 milioni (Shilingi 22, 183, 027) na kuongeza kuwa aliificha takriban miezi miwili kabla ya kuichomoa na kuweka katika kidole cha mrembo wake huyo.

Hadi sasa, wawili hao wamefanya vikao tofauti ikiwamo hafla ya kupeleka mahari miezi mitatu iliyopita, sherehe iliyofanyika nyumbani kwao Anerlisa, Naivasha, Kaunti ya Nakuru.