Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
 Baadhi ya Washiriki wa Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 Mkaazi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Bibi Jacquiline Mahon akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA} kwenye Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu.
 Baadhi ya Viongozi wa Serikali walioshiriki kwenye Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akitoa salamu za Wizara ya Afya katika Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Watendaji wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa waliobahatika kushuhudia Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu.
 Balozi Seif akimpongeza Mmoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Al – Ahzar cha Nchini Misri kutokana na uamuzi wao wa kusaidia kufanyika kwa Mjadala huo wa Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu. Kati kati yao anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman. Picha na – OMPR – ZNZ.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al - Hajj Dr. Ali Mohamed Shein alisema maradhi mengi yanayowakumba Watoto yakikosa kushughulikiwa kwa Tiba sahihi katika hatua za awali huendelea kubakia kuwa matatizo ya kudumu katika maisha yao ya baadae.

Alitanabahisha kwamba Mtoto asiye na afya njema kamwe hawezi kukua vizuri jambo ambalo huathiri ustawi wa maisha yake na baadhi ya wakati hushindwa kufanya vizuri katika masomo na kukosa ushirikiano mwema na wanafunzi wenzake.

Dr. Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90% ya Watoto walio na umri wa chini ya Mwaka Mmoja hunyonyeshwa, lakini ni Watoto 37 kati ya Watoto 100 walio na umri kati ya Mwaka Mmoja hadi Miwili ndio wanaonyonyeshwa kabla ya Mama zao kubeba ujauzito mwengine.

Dr. Shein alisema hali hiyo inaonyesha wazi kwamba Jamii inahitaji kuimarisha Utamaduni muhimu kwa Wanawake wananyonyesha kwa kipindi kinachokubalika kama wanavyoifanya kina Mama walio wengi hivi sasa ili kuimarisha Afya za Watoto.

Alisema asilimia 30% ya vifo vinavyotokana na Uzazi vinaweza kupungua kama Jamii itakuwa na matumizi mazuri ya huduma za Uzazi wa Mpangilio, na hii inajionyesha wazi elimu ya mpango huu kuanza kuwafikia Wananchi kutokana na Takwimu zinazothibitisha Wanawake 28 kati ya 100 hutaka kutumia huduma hizo.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba njia hizo hawazipati kutokana na sababu tofauti ikiwemo ukosefu wa Taarifa sahihi za Afya ya Uzazi dhana zisizokuwa sahihi kuhusu njia ya Uzazi wa Mpangilio pamoja na ufahamu mdogo wa Elimu ya Dini juu ya suala la zima la uzazi wa mpangilio katika Uislamu.

Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya Watu wanaopotosha maana halisi ya Uzazi wa mpangilio kwa kuvihusisha vitendo vya utoaji wa mimba bila ya sababu zilizoruhusiwa za afya.

Alisema hali hii imewafanya baadhi ya watu hasa akina Mama wakose hamu ya kutafuta na kupata taaluma sahihi juu ya suala hilo ambalo hata dhamira ya Serikali Kuu haihusiani na njia yoyote ya utoaji mimba kwa njia ye yote ile.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitahadharisha na kuonya kwamba ni kosa la jinai kufuatana na Sheria ya Makosa ya Jinai ya Mwaka 2017. Hivyo Serikali inapinga vikali utoaji Mimba na vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya Watoto wa rika zote.

Akigusia suala la unyonyeshwaji kwa Watoto, Dr. Ali Mohamed Shein alisema tafiti nyingi zimethibitisha kwamba Mama anaponyonyesha uwezo wake wa kuchukuwa mimba unapungua kutokana na mabadiliko ya kemikali zinazofanya kazi ya kusaidia mfumo wa kiwiliwili ufanye kazi vyema.

Alisema hayo ni masuala muhimu yanayopaswa Jamii hasa Kina Baba kuyafahamu iwapo kutafanyika Mijadala itayotoa elimu itakayohusiana na masuala mazima ya mfumo wa uzazi wa mpangilio unaokubalika Kisayansi sambamba na Kidini.

Dr. Ali Mohamed Shein aliwaeleza washiriki wa Mjadala huo wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpangilio katika Uislamu kwamba Serikali inatambua mafanikio makubwa katika uimarishaji wa Afya za Wananchi yanategemea usimamizi mzuri wa Mipango ya Taifa.

Alisema juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Afya ya akina Mama na Watoto zimelenga katika kupunguza idadi ya Vifo vya Mama na Watoto vinayotokana na masuala yote ya uzazi.

Hata Hivyo Dr. Shein alifahamisha kwamba Sera, Maendeleo na Sheria zilizopo za Nchi zimetoa uhuru kwa Wananchi kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu namna bora ya kupanga Uzazi kwa kutegemea Imani za Kidini, Utamaduni na Mipango ya Maendeleo ya Familia.

Alisisitiza kwamba suala la Uzazi wa Mpangilo bado linaendelea kuwa ni suala la hiari kwa Wanafamilia kadri watakavyo, wanandoa kufuatana na Imani za Dini na Mitazamo yao.

Dr. Shein alitanabahisha kwamba bado wapo baadhi ya Wananchi wenye hitilafu ya mawazo inayowapa taabu ya kutofautisha kati ya Uzazi na Mpango na uhuru wa kuzaa hasa pale Serikali inapoweka Mikakati ya kutekeleza Uzazi huo ambapo Watu hao hufikiria kuzuiwa kuzaa.

“ Serikali ni Watu, walioichagua kwa ajili yao , kwa maslahi yao na kwa madhumuni yao. Serikali si ya Mtu Mmoja, bali ya Watu wote. Hivyo suala la uzazi ni la lazima kwa Maendeleo yetu” Alisisitiza Rais wa Zanzibar.

Alisema Taifa linahitaji kuwa na kiazi kipya kitakacho chukuwa urithi wa kile chilichopo hivi sasa kwa lengo la kuimarisha nguvu kazi kadri ya Uchumi wake unavyoendelea kukua.

“ Tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunazaa , ili pawe na warithi wa Taifa letu. Imani hii haipingani hata chembe na mafundisho na miongozo ya Dini”. Alifafanua Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kwamba Serikali Kuu imeweka utaratibu mzuri wa kuzitambua na kuzikubali ndoa zote zilizofungwa kwa misingi ya Kiislamu na kwa taratibu za Dini Nyengine zinazojuilikana na kutambuliwa katika Sheria za Nchi.

Alisema kinachofanyika kwa Serikali ni kufanya jitihada kubwa katika kutoa Elimu ya Uzazi wa Mpangilio unaozingatia mafundisho ya Dini zote zilizopo pamoja na maadili na Utamaduni wa Watu wa Zanzibar.

Mapema kitoa Taarifa ya Mjadala huo wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpangilio katika Uislamu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdullah alisema asilimia 14% ya Wananchi wote Visiwani Zanzibar ndio wanaotumia Uzazi wa Mpangilio hali inayotoa mwana kwa Akina Mama wengi kuendelea na uzazi wa papo kwa papo unaoleta athari kwa afya za Mama na Mtoto.

Bibi Asha alisema changamoto hiyo inatokana na mtazamo wa Jamii katika kuihusisha Dini na masuala ya Uzazi wa Mpangilio.

Alisema juhudi za kushirikisha Viongozi wa Kidini zimesaidia kwa kiasi kikubwa kampeni ya kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vinavyosababisha maambukizo ya Ukimwi Nchini.

Bibi Asha Ali Abdullah alisema ni vyema Kampeni hiyo iliyohusisha Viongozi wa Kidini kwa sasa ikaelekezwa katika kampeni ya kupunguza vifo vya Akina Mama kwa kuzingatia zaidi Uzazi wa Mpangilio.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alilipongeza na kulishuruku Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA},Taasisi ya Chuo Kikuu cha Aga Khan pamoja na Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al - Azhar cha Nchini Misri kwa moyo wao wa kusaidia Taaluma juu ya uzazi wa Mpangilio.

Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA}, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Bibi Jacquiline Mahon alisema mchango mkubwa uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti Mkuu na Wizara ya Afya Zanzibar umesaidia kufanikisha Mjadala wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpangilio katika Uislamu.

Bibi Jacquiline alisema kitendo cha kufanywa mjadala huo kitatoa fursa kwa Wananchi walio wengi kupata Taaluma ya uelewa juu ya uhumimu wa kuimarisha Uzazi wa Mpangilio hasa ikizingatiwa kwamba hadi sasa Zanzibar ina asilimia 14% ya Watu wanaotumia Uzazi huo.

Alisema asilimia hiyo ndogo ikiachiwa kuendelea upo uwezekano wa kutoa mwanya wa kukaribisha vifo vya papo kwa papo vya Akina Mama na Watoto vitavyoendelea kutokea kutokana na kutokuwa na mipango madhubuti ya kuwapa haki yao Akina Mama na Watoto ya kubeba Mimba na Kunyonyeshwa kwa mpangilio unaokubalika Kiafya.

“ Kwa tafiti zilizowazi ni thuluthi Moja tu ya Akina Mama Visiwani Zanzibar wanaozingatia umuhimu wa Uzazi wa Mpangilio kwa kuchelewesha Mimba moja hadi kutunga Mimba nyengine”. Alisisitiza Bibi Jacquiline.

Mwakilishi Mkaazi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA}, Nchini Tanzania Bibi Jacquiline Mahon aliupongeza Uongozi wa Vyuo Vikuu vya Aga Khan na Al – Azhar ya Misri kwa ushirikiano wao na Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Idadi ya Watu.

Alisema Ushirikiano huo umesaidia kuchapisha vitabu mbali mbali vinavyosaidia kutoa elimu inayohusiana na Uzazi wa Mpangilio ambayo hutoa muelekeo wa kuzingatia maisha bora yanayofaa kuendelezwa na wana Familia .

Bibi Jacquiline aliithibitishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo katika Mipango na Miradi yake ya Maendeleo hasa Dira ya 2020 pamoja na mapambano ya vita dhidi ya kupunguza vifo vya Akina Mama na Watoto.