Mshauri Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa, kuonekana pamoja kwa viongozi wawil vya vyama vya siasa vya upinzani, Zitto Kabwe (ACT) na Tundu Lissu (CHADEMA), kumewapa nguvu kuelekea uchaguzi wa 2020.Maalim ameeleza kuwa wawili hao waliokutana nchini Ubelgiji ambako Tundu Lissu anaendelea na matibabu, wameonesha njia nzuri.

''Zitto Kabwe na Tundu Lissu wametupa faraja na kutuonesha njia kuelekea 2020. Nawapongeza na kuwatia moyo kutekeleza wajibu wa kihistoria kwa Tanzania wakati tunaelekea uchaguzi mkuu wa 2020 ambao ni uchaguzi muhimu kuliko chaguzi zote katika kuamua mustakabali wa Tanzania''.

Zitto Kabwe alirusha video mtandaoni ikionesha yupo na Tundu Lissu, wakitembea kwenye mitaa huko Ubelgiji huku wakisema mwanasheria huyo wa CHADEMA yupo tayari kurejea nchini.

Kwa mujibu wa ratiba aliyowahi kuitoa mwenyewe, Tundu Lissu atarejea nchini Septemba 7, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoondoka kwenda kutibiwa mwaka 2017, kutokana na kujeruhiwa kwa kupigwa risasi mkoani Dodoma.