MWANAMAMA mjasiriamali wa Uganda mwenye maskani yake kwa Madiba nchini Afrika Kusini, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, wikiendi iliyopita alitua Bongo kimyakimya na kumpa tano Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’.



Kupitia akaunti yake ya Mtandao wa SnapChat, Zari ambaye mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alitupia video na picha akiwa kwenye ndege akitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar na kuumwagia sifa uwanja huo, eneo la Terminal 3.



Katika maelezo aliyoambatanisha na video na picha ya mawingu wakati ndege ikitua, Zari alipongeza juhudi za JPM ambaye amefanikisha kukamilika kwa uwanja huo ambao aliuzindua hivi karibuni.

Zari alipongeza uwanja huo kwa jinsi ulivyo wa kisasa na wa kimataifa ukilinganisha na viwanja vingine vikubwa vya ndege duniani.

“Congratulation to Julius Nyerere International Airport Terminal 3,” alisema Zari na kuweka dole gumba kuashiria kukubali kazi nzuri ambayo imefanywa na JPM.

Tofauti na ilivyozoeleka ambapo akitua Bongo huwa na ‘matangazo’ mengi, safari hii Zari alitua kimyakimya na hakukuwa na shamrashamra kama wakati mwingine.

Nusanusa ya Gazeti la Ijumaa Wikienda ilibaini kuwa, Zari alitinga Bongo kwa shughuli zake za ubalozi na matangazo ya pampers za watoto ambazo huwa ana mkataba mrefu.

Pia gazeti hili linafahamu kwamba baada ya kutua Dar, Zari alifikia kwenye hoteli ya kifahari ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro kisha kupiga zake matangazo huku akifurahia hali ya hewa ya Jiji la Dar.

Kwa mujibu wa wananzengo, Zari hakuwa na mbwembwe na ulinzi kama zamani kwani nafasi yake kwa Diamond au Mondi imechukuliwa na mtangazaji kutoka Kenya, Tanasha Donna Oketch na tayari amemzalia mtoto wa kiume jamaa huyo.

Kwa upande wa shughuli za maendeleo, JPM amekuwa akipongezwa kwa jitihada zake za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mbali na hiyo Terminal 3, miradi mingine mikubwa ya kimaendeleo inayosimamiwa na Serikali ya JPM ni pamoja na mrafi mkuwa wa umeme wa Rufiji, reli ya kisasa ya SGR, madaraja, viwanda na barabara katika kila kona ya Tanzania.