Ujumbe Kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar ukiwa katika mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi ambaye katika mazungumzo hayo alieleza kwamba Ofisi hizo mbili zinakusudia kuanzisha utaratibu au mfumo rasmi wa mashirikiano na uhusiano baina ya Taasisi hizo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi akizungumza na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar Bw. Mzee Alli Haji ambaye aliongoza ujumbe wa watu sita katika ziara yao ya kuitembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ( Bara) kwa madhumini ya kubadilishana mawazo na uzoefu na kuangalia maeneo ya kushirikiana hususani kwa yale yenye sura ya Muungano ikiwamo Mikataba ya Kikanda na Kimataifa.

Na Mwandishi Maalum, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) Profesa Adelardus Kilangi amesema, Baada ya majadiliano na mashauriano ya kina na Mwenzake, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mhe.Said Hassan Said wanakusudia kuanzisha utaratibu rasmi utakaoratibu mashirikiano na mahusiano baina ya Ofisi hizo mbili.

Ameyasema hayo siku ya Jumatano jijini Dodoma, wakati alipokutana na kuwa na mazungumzo na Ujumbe wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Serikali wa Zanzibar ulioongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Mzee Alli Haji.

AG kilangi ameuambia ujumbe huo kwamba, ingawa Ofisi hizo hivi sasa zinashirikiana katika masuala mbalimbali yenye maslahi mapana kwa kwa pande zote mbili za Muungano, ushirikiano huo haujawekewa utaratibu unaoeleweka

"Tumeliona hili mimi na mwenzangu na kwa kweli tunashirikiana vizuri sana lakini katika namna ambayo ni ad hoc, sasa tumekubaliana na kudhamiria kuwa na utaratibu rasmi utakaosaidia na kurahisisha mashirikiano haya ili kwayo tuweze kuzishauri vema serikali zetu na hatimaye ziwatumike vizuri na kwa tija wananchi wake"

Akaongeza kuwa kwa Watumishi wa Ofisi hizo mbili, kutembeleana, kubadilishana mawazo, uzoefu na kupeana ushauri kunaimiarisha na kuboresha utekelezaji wa majukumu.

Kauli ya AG Kilangi inatoka na hoja iliyotolewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar kwamba, moja ya madhumuni ya ziara yao iliyowafikisha Ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ( Bara) ni kujadiliana namna ya kukuza, kuendeleza na kudumisha uhusiano na mashirikiano baina ya Ofisi hizo.

Profesa Kilangi akatoa mfano kwa kusema kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limejiwekea utaratibu au mfumo wa kuwa na mashauriano na Serikali ya Zanzibar pale linapotaka kutunga sheria ambayo inagusa pande zote mbili za Muungano

Naibu Mwanasheria huyo aliongeza kuwa Ofisi zote mbili zinajenga nyumba moja kwa hiyo suala la uhusiano na masharikiano haliepukiki.

Akasisitiza kwamba, endapo Ofisi hizo zitashirikiana kwa karibu, hata zile hoja zinazojitokeza kama kero za Muungano zitaweza kushughulikiwa vizuri zaidi ikiwa Wanasheria Wakuu hao wa Serikali watakuwa na utaratibu rasmi wa kukutana na kujadiliana.

Pamoja na kusudio la kuweka rasmi utaratibu wa kushirikiana, Ofisi za Wanasheria Wakuu wa Serikali Bara na Zanzibar pia zimekubaliana kuangalia namna ya zitakavyobadilishana uzoefu katika maeneo ya uandishi wa Sheria,maandalizi na uhakiki wa mikataba hususani ile ya Kikanda na Kimataifa na ambayo utekelezaji wake utahusu pande zote mbili za Muungano.

Taasisi hizo pia zimekubalianakuangalia pia namna zitakavyoshirikiana katika kuwajengea uwezo na maarifa Mawakili wa Serikali na watumishi wengine kwa kushirikiana katika nafasi za mafunzo ya ndani na nje ya nje.

Kuhusu eneo hilo la mafunzo na kuwajengea uwezo watumishi wa Taasisi hizo, Profesa Kilangi amesema Zanzibar inaouzeofu mkubwa katika baadhi ya maeneo ambayo pia yanahistoria ndefu.

Aidha Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bw. Mzee Alli Haji pia alishauri kwamba, Taasisi hizo mbili pia zinaweza kushirikiana kwa kubadilishana mawazo na uzoefu katika kesi ambazo zina sura ya Muungano. Hoja ambayo imeungwa Mkono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi.