Wanafunzi wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mwanafunzi Muddy Muswadiku aliyekuwa anasoma katika shule ya sekondari Katoro Islamic Seminary ya Mkoani Kagera wameruhusiwa kuendele kujisomea wakiwa gerezani wakiwa wanajiandaa na mtiahani wa kidato cha nne utakao fanyika  mnamo Novemba 4,mwaka huu nchini.

Ruhusa hiyo imetolewa na mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera baada ya mmoja wa watuhumiwa wa kesi hiyo  Majaliwa Abdu (mwalimu) kuwasilisha maombi ya kuwaruhusu wanafunzi hao kusomea gerezani huku wakijiandaa na mtihani, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili mahakamani hapo.

Kufuatia ombi hilo, Wakili wa Serikali mkoani Kagera, Haruna Shomari amesema watuhumiwa hao watapatiwa hati hiyo ya mashtaka   na pia vitu kama madaftari, vitabu na kalamu wanaruhusiwa kuwa navyo gerezani.

Katika kesi hiyo pia idadi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera, imeongezeka baada ya wanafunzi wengine wawili kuongezwa katika shitaka hilo.

Wanafunzi waliongezwa ni Sharifu Amri (19) na Fahadi Abdulazizi Kamaga (20) na kusababisha idadi ya watuhumiwa kufikia wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mlinzi mmoja wa shule hiyo.

Kesi hiyo ya mauji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage, imetajwa kwa mara ya pili Jana katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera.

Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wanafunzi Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35) mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Septemba 30 mwaka huu ambapo pia itatajwa tena kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shitaka hilo.

Wakili Shomari amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuwa wanafunzi walioongezwa, nao wamebainika walishiriki kumpiga Mudy (marehemu).

“Katika upelelezi tunaoendelea kuifanya tulibaini kuwa pia wanafunzi hao wawili walioongezwa nao walishiriki kumpiga marehemu (Mudy) wakati huo huo bado upelelezi unaendelea,” alisema Shomari.

Mauji hayo yalitokea Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi kesi itakapo tajwa tena