Na Kilo Mgaya, Masasi - Mtwara

Meneja wa Kanda ya Kusini Benki ya CRDB Bi. Jeniffer Tondi amevihimiza vyama vya ushirika kanda ya kusini inayohusisha mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB katika uwezeshaji sekta ya kilimo.

Akizungumza katika kongamano la uwezeshaji sekta ya kilimo lililoandaliwa na Benki ya CRDB na kuhudhuriwa  na vyama vya ushirika zaidi ya 42 katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Bi. Tondi alisema Benki ya CRDB imeweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha inaisaidia Serikali kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini ili kusaidia kufikia malengo ya kujenga uchumi wa kati wa viwanda.

“Katika uwezeshaji wa sekta ya Kilimo Benki yetu imekuja na kauli mbiu inayosema Kilimo chetu, Viwanda vyetu, Uchumi Wetu, ambapo tumejikita katika maeneo makuu matatu ikiwamo mikopo ya pembejeo na uendeshaji, uunganishwaji na masoko pamoja na kutoa elimu ya mambo ya fedha na uwekezaji,” alisema Bi. Tondi.
Akizungumzia uwezeshaji katika zao la korosho kwa mikoa ya kanda ya kusini, Bi Tondi alisema Benki ya CRDB mwaka jana pekee ilitoa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 16.9, huku akieleza kuwa fedha hizo zimeelekezwa katika katika ununuzi wa pembejo za kilimo pamoja  ununuzi wa magunia ya kuhifadhia korosho kwa vyama vya ushirika vya msingi.

Akizungumza katika kongamano hilo Meneja wa tawi la Benki ya CRDB, Amani Madale aliwasisitiza wakulima kutumia fursa ya akaunti ya FahariKilimo katika kupokea malipo yao, huku akisema kuwa akaunti hiyo imezingatia zaidi mahitaji ya wakulima ambapo hufunguliwa pasipo kuwa na gharama zozote za uendeshaji.

“Mkulima anapofungua akaunti hii anaunganishwa moja kwa moja na huduma ya SimBanking inayomuwezesha kufanya miamala yote ya kifedha kupitia simu yake ya mkononi, lakini pia kupitia kadi yake ya TemboCard mkulima ataweza kupata huduma kupitia mawakala wetu wa CRDB Wakala ambao wapo mpaka vijijini ambapo ndipo wakulima wengi walipo,” aliongezea Madale huku akivitaka vyama vya ushirika kuchangamkia fursa ya CRDB Wakala.

Kwa upande wake Meneja wa Chama Kikuu cha Uchirika Mtwara na Masasi (MAMCU), Joseph MMole aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa kongamano hilo la uwezeshaji sekta ya kilimo huku akisema kongamano hilo litakwenda kuwahamasisha wakulima wengi kujitokeza kuchukua mikopo ya pembejeo na hivyo kuwawezesha kufanya kilimo cha kisasa zaidi.

Mbali na fursa za mikopo ya kilimo na akaunti ya FahariKilimo, wakulima pia walihamasishwa kujitokeza kuchangamkia fursa za huduma za bima, mikopo ya nyumba, pikipiki, bajaji ikilenga kuboresha maisha yao, huku pia wakihamasishwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika hisa za Benki ya CRDB ili kujiongezea kipato.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kusini, Jeniffer Tondi akizungumza na wawakilishi wa vyama vya ushirika vya msingi katika kongamano la uwezeshaji sekta ya kilimo wilayani Masasi lililofanyika katika ukimbi wa mikutano wa hoteli ya Rock City. Benki ya CRDB imewahimiza wakulima kuchangamkia fursa za mikopo ya kilimo kuboresha kilimo chao huku ikiwataka wakulima kujiunga na akaunti ya FahariKulimo ambayo haina gharama yoyote ya uendeshaji na hivyo kumpa mkulima unafuu.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Masasi, Amani Madale akizungumza na wawakilishi wa vyama vya ushirika vya msingi katika kongamano la uwezeshaji sekta ya kilimo wilayani Masasi lililofanyika katika ukimbi wa mikutano wa hoteli ya Rock City. 
Sehemu ya Washiri wa kongamano la uwezeshaji sekta ya kilimo liloandaliwa na Benki ya CRDB wilayani Masasi, wakifatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa. 
Baadhi ya Washiri wa kongamano la uwezeshaji sekta ya kilimo liloandaliwa na Benki ya CRDB wilayani Masasi, wakiuliza maswali.