KAMA ulikuwa unajiuliza kilichokuwa kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii wikiendi iliyopita huku baadhi ya watu wakidai ni ndoa ya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na mchumba’ke, Sarah Michelotti, Ijumaa Wikienda lina ukweli.  Awali zilisambaa picha zikimuonesha Harmonize au Harmon a Sarah wakiwa na cheti kilichoonesha wamefunga ndoa ya Serikali (bomani), zoezi ambalo lilidaiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar kisha kufuatiwa na tafrija iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena.

Katikati ya mkanganyiko huo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Harmo ambaye alielekeza kila kitu aulizwe meneja wake, Beauty Mmari ‘Mjerumani’. Katika mazungumzo na gazeti hili, Mjerumani alisema kuwa Harmo hawezi kufunga ndoa halafu jiji lisitikisike kwa kuwa hakuna asiyemjua.

“Hakukuwa na ndoa yoyote pale. Kinachoendelea ni kwamba Harmonize ana-shoot video ya wimbo mpya ambao unahusiana na mambo ya harusi kama ule ambao Diamond (mwanamuziki Nasibu Abdul) ali-shoot na Zari (Iyena).

“Wimbo huo wa Harmonize unaitwa Marry Me, lakini watu walivyoona zile picha zikisambaa, wakatafsiri kuwa ni ndoa. “Harmonize hawezi kufunga ndoa halafu mji usitikisike kwa kuwa kuna watu wengi ambao watatakiwa kuwepo kwenye ndoa kama ingekuwa ndoa kweli.

“Lile tukio linaonesha watu wachache ambao wamehudhuria. “Kwa hiyo niweke wazi tu kuwa ni wimbo na siyo ndoa,” alisema Mjerumani. Mwishoni mwa mwaka uliopita Harmo alimchumbia Sarah nyumbani kwao nchini Italia hivyo kinachosubiriwa ni tukio kubwa la ndoa.

Stori: Neema Adrian