Na Jumbe Ismailly MKALAMA
UJENZI wa daraja la Mto Sibiti uliopo Kijiji cha Nyahaa,Kata ya Mpambala,wilayani Mkalama,Mkoani Singida lenye urefu wa mita 82 umeanza kuhujumiwa na watu wasiojulikana kwa kuondoa kifaa kinachotambulika kitaalamu kwa jina la EXPANSION JOINT kinachosaidia kuzuai daraja hilo lisitanuke.

Akizungumza kwa njia ya simu,kaimu meneja wa Wakala wa Barabara (TANROAD) Mkoa wa Singida,Mhandisi Matare Masige alifafanua kwamba pamoja na serikali kutumia mabilioni ya fedha kugharamia ujenzi wa daraja hilo,lakini baadhi ya wananchi wameanza kufanya hujuma kwa kuiba baadhi ya vifaa vilivyowekwa katika daraja hilo.

Alibainisha kaimu meneja huyo kwamba licha ya serikali kupeleka askari kwa ajili ya kulinda daraja hilo lisihujumiwe lakini katika hali ya kushangaza,kusikitisha na kuleta sintofahamu,kwani katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Raisi Dkt.John Pombe Magufuli alipoweka jiwe la msingi uharibifu umeanza kujitokeza.

Alipotakiwa kuzungumzia hujuma zilizoanza kujitokeza huku kukiwa na taarifa kwamba jeshi hilo lilipeleka askari kwa ajili ya kulinda daraja hilo,akizungumza kwa njia ya simu akiwa katika safari za kikazi,Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida,ASP.Sweetbert Njewike alikiri kupeleka askari kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa adaraja hilo.

Hata hivyo ACP Njewike alisisitiza kwamba daraja hilo limekuwa likilindwa kwa zamu kati ya askari wa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu na anaamini kwamba Mkuu wa polisi wilaya ya Mkalama alikuwa akaisimamia zoezi hilo kikamilifu ili madhara yeyote yale yasiweze kutokea.

Aidha Kamanda huyo wa jeshi la polisi aliweka bayana kwamba kwa amujibu wa maelezo ya kitaalamu aliyopewa na Kaimu Meneja wa TANROAD Mkoa wa Singida ni kwamba kifaa kilichohujumiwa hakiwezi kuleta madhara yeyote ile kwenye daraja hilo wakati vyombo vya moto vitakapoanza rasmi kutumia barabara hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye daraja hilo,baadhi ya wananchi na viongozi wa kata ya Mpambala walionyesha kusikitishwa na hujuma zilizofanywa za kuiba kifaa hicho chenye umuhimu mkubwa katika daraja hilo.

 Diwani wa kata ya Mpambala,Boazi Hasani Ndandutwa akizungumzia tuhuma za askari waliokwenda huko kwa ajili ya kulinda daraja hilo kufanyakazi za kukamata vyombo vya moto siku yam nada wa Bukundi alikiri kuwakuta askari hao kila siku ya jumatano kunapokuwa na mnada.

“Kwa akweli kila wakati nilikuwa anapita kwenda Bukundi nilikuwa nawakuta askari wapo hapa darajani,lakini kwa siku za katikati mwa wiki au mwanzoni mwa wiki kiukweli mara nyingi nilikuwa sipiti lakini siku ya jumatano ni kila jumatano wanakuwa huku kwenye daraja,”alifafanua diwani huyo.

Hata hivyo Boazi alionekana kushangazwa na uharibifu huo ulioanza kutokea katika daraja hilo alishindwa kufahamu iwapo uharibifu huo unafanyika wakati wa usiku au mchana na hivyo kuahidi kwamba atalazimika kuwatafuta na kuwasisitiza askari ili waweze kuona uharibifu unaotokea ili nao waweze kuchukua nafasi yao kwa kuimaraisha ulinzi zaidi.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mwanga Jasia Jacksoni Shabani alisisitiza kwamba iwapo kuna askari waliopelekwa kulinda daraja na wao kuamua kufanya kazi nyingine serikali isisite kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na kuzembea hadi daraja limeanza kuhujumiwa.

“Sawa askari wanatakiwa wachukuliwe sheria kwa sababu kama wamepewa dhamana ya kulinda hili daraja na sasa hivi hawajafanikiwa kufika hapa ni mojawapo ya makosa askari wanayoyafanya,cha msingi inatakiwa hawa maaskari watafutwe sheria ambazo zinahitajika kuchukuliwa juu yao ili wasije tena wakakosa kufanya ulinzi katika hili daraja.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mhandis Jacksoni Masaka licha ya kukiri kupata taarifa za kuhujumiwa kwa daraja hilo kutoka kwa meneja wa tanroad mkoa wa singida lakini alibainisha kuwa kamati ya ulinzi na usalama ilishamwagiza kamanda wa polisi wa wilaya kupeleka askari kwa ajili ya ulinzi wa daraja hilo.

“Daraja hili linalindwa na polisi wanafanya patro mara kwa mara kwa hiyo kamati ya ulinzi na usalama ilishamwagiza ocd ahakikishe anapeleka kule askari,tatizo lake ocd wakati mwingine anakuwa hana gari la uhakika,gari lake ni bovu wakati mwingine linakuwa lina shida ya matairi na kule kituo cha Ibaga hawana gari la kituo,kwa hiyo wanalazimika kutumia pikipiki mara kwa mara kwenda Sibiti kitu ambacho kinakuwa kina gharama fulani kwa askari.”alisisitiza mkuu wa wilaya huyo.
 Mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mhandisi Jacksobi Masaka(aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa hujuma zinafanywa kwenye daraja la mto Sibiti kwamba kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imemwagiza OCD kuhakikisha anapeleka askari kulinda daraja hilo. Daraja lililojengwa katika mto Sibiti ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu pamoja na bidhaa mbali mbali kupeleka kwenye masoko ya biashara ya ndani na nje ya nchi.


 maeneo ya daraja la mto Sibiti yaliyoanza kuhujumiwa na watu wasiojulikana kwa kuchukua kifaa kinachojulikana kwa jina la kitaalamu la "EXPANSION JOINT" kinachosaidia daraja kutotanuka.