Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ameonesha kuvurugwa na wingi wa makato ya kodi anazotozwa kwenye matamasha yake ya Wasafi Festival na show zake nyingine za ndani.

Diamond akiongea na maafisa TRA mkoani Iringa, Aliwauliza bei ya kubandika bango (Posters) yenye ukubwa wa A4 ni shilingi ngapi?.

TRA walimjibu Diamond kwa kusema kuwa, Viwango vya bei za Posters inategemea na ukubwa wa bango lenyewe na eneo husika kwa kutumia ‘By Law’ zinzotumika eneo hilo.

Diamond aliendelea kuhoji kuhusu bei ya mabango hayo kwa kutoa mfano, Ambapo alisema kuwa mwaka huu walienda kupiga show Kahama mkoani Shinyanga na walipoenda kufuatilia bei za kupandika mabango (Posters) aliambiwa na TRA wilayani humo kuwa kila bango litatozwa Tsh elfu 3 kwa siku.

Amesema yeye alipanga kuweka mabango 3,000 (Posters 3000) kwa siku 14, Ambapo kwa bei hiyo ilimpasa alipe Tsh Milioni 126 kwa kuweka mabango tu mjini Kahama.

Diamond na waandaaji wenzake waligoma kulipa fedha hiyo, Kwani show hiyo ilikuwa na kiingilio cha Tsh elfu 10 jambo ambalo fedha zote zingeishia kwenye mabango.

Maafisa hao wa TRA ambao walikuwa kwenye banda la Maonesho ya utalii mjini Iringa, Walimjibu kuwa hicho kitu hakiwezekani ni bei kubwa sana, Na kisha maafisa hao walichukua maelezo kutoka kwa Diamond wakimtaka ataje mkoa aliofanyiwa hivyo ili kufikisha malalamiko yake kwa wahusika.

Diamond aliendelea kuhoji kwa kuuliza, “Kwa mfano sisi kama Wasafi Limited kila mwisho wa mwaka tunalipa kodi zetu sawia kabisa. Na miongoni mwa shughuli nyingine tunazozifanya ni pamoja na kuandaa show za Wasafi Festival. Je, unatakiwa ulipe ile asilimia 18 mwisho wa mwaka au nilipe pale pale ninapomaliza show ambayo tumeandaa sisi wenyewe.?”

TRA wamemwambia kuwa kama tamasha limeandaliwa na Wasafi Limited, Hawezi kukatwa 18% palepale baada ya show kumalizika na badala yake, Kinachotakiwa ni yeye na TRA kutunza nyaraka zote za malipo na gharama zote zilizotumika na kodi atakatwa 18% mwishoni wa mwaka kama kampuni.