Serikali imesema haitasita kuwang’oa kwenye nafasi zao Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Idara na Wataalam wa watakaoshindwa kuubeba Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF), kwenye ajenda za vikao kazi vyao.

Hayo yalisemwa wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Dorothy Gwajima wakati wa kikao kazi kati yake, mkuu wa wilaya, mkurugenzi na wakuu wa idara za wilaya ya Mkuranga.

Alisema hivi sasa Serikali ipo kwenye mkakati wa kuiboresha na kuitekeleza TASAF mpya hivyo ni lazima kila idara ihakikishe walengwa wa mpango huo wanafuatiliwa kuanzia kwenye afya na shughuli zao za kiuchumi.

“Walengwa hawa wanaitwa maskini kwa sababu ya uchumi lakini wanazo nguvu na akili za kufanyakazi… ndio maana serikali imeleta TASAF kuwapa ‘starter’ wakipata chakula waende wakafanye shughuli za kiuchumi kwenye eneo lao.

“Taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda hatuwezi kufika ikiwa kuna watu wanasubiri kupewa tu, hapa tunawajengea na uwezo pia kiuchumi.

“Nasisitiza kwamba lazima vikao 12 vya CMT viwe na ajenda 12 za TASAF na hili nitalisimamia kwa hakika nitapita kwenye halmashauri zote 184 za nchi hii. Nitakayekutana nae anaibagua TASAF huyo atakuwa hatoshi na inshaallah nchi hii ina watu wenye uwezo tutamtoa tutamuweka anayeuelewa mpango huu,” alisema Dk. Dorothy.

Alisisitiza kwamba TASAF ni mgoma inayotakiwa kuchezwa na wote kuanzia kitongoji hadi taifa huku maofisa ustawi wa jamii, afya, elimu, kilimo, mifugo, sheria na uchumi wakiwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu.

“Kwenye hili sitakubali kuona mnamuangusha Rais John Magufuli nitalisimamia hili na mazuri yote ya TASAF yaonekane… wanasema maji madogo ndio yanayozamisha watu usilidharau hili litakuzamisha,” alisisitiza Dk. Gwajima ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya TASAF taifa.

Akizungumzia Ushiriki wa Halmashauri ya Mkuranga, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Mhandisi Mshana Munde alisema baada ya kupewa elimu sahihi kuhusu TASAF amelazimika kutengeneza sheria ndogo ili Mratibu wa TASAF aingie kwenye vikao vya utendaji kila mwezi.

“Tumekuelewa na sisi kwenye vikao vyetu tumerekebisha sheria ili Mratibu wa TASAF aingie na tunapokea taarifa yake inakuwa rasmi kwenye taarifa za halmashauri, awali jambo hili halikuwepo,” alisema Munde.