AMISSI Tambwe ni mmoja kati ya washambuliaji wenye rekodi na historia kubwa katika Ligi Kuu Bara kwa kipindi cha miaka sita aliyocheza ligi hiyo kutokana na ubora wake wa kufumania nyavu.

Tambwe aliingia Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2013, alipojiunga na Simba akitokea Vital’O ya nchini kwao Burundi.



Alidumu Simba kwa msimu mmoja na nusu, akatemwa na kuibukia Yanga. Hiyo ilikuwa ni katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2014/15.


Amissi Tambwe (kulia) akiwa na mwandishi wa makala haya, Ibrahim Mussa (katikati) na mkewe

Gazeti la Championi Ijumaa limefanikiwa kumpata mshambuliaji huyo akiwa katika Jiji la Bujumbura nchini hapa muda mchache kabla ya kukwea ndege kuelekea nchini Oman tayari kuanza kazi katika timu yake mpya ya Fanja aliyojiunga nayo hivi karibuni baada ya kuachwa na Yanga.



Licha ya kuwa na makazi yake yenye uhakika nchini hapa, lakini gazeti hili halikufanikiwa kufi ka nyumbani kwa mshambuliaji huyo kutokana na kubanwa na ratiba ya safari yake na badala yake alikuwa kwa rafi ki yake ambaye alikwenda kumuaga kabla ya kuondoka.

UMECHEZA TANZANIA KWA MIAKA SITA, UMEJIFUNZA NINI?

“Tanzania nimejifunza mambo mengi sana kwa sababu kuishi katika nchi ya watu kwa kipindi cha miaka sita siyo jambo dogo kabisa. “Unajua wakati nacheza hapa kwetu, nilikuwa nimezoea kula ugali wa muhogo tu lakini nilivyokuja Tanzania nilikuta mnakula ugali wa sembe ambao umepelekea niuchukie ugali wa muhogo. “Binafsi najua kwamba Tanzania ni nyumbani kwa sababu sehemu ambayo natokea mimi hapa Burundi kuelekea Kigoma ni mwendo wa dakika 30 tu.

JAMBO GANI HUWEZI KULISAHAU WAKATI UNAONDOKA SIMBA?

“Unajua kwanza Simba sikuondoka kwa kupenda lakini kutokana na hali iliyotokea ilinibidi niondoke kwa kuwa viongozi hawakuwa na ukweli wowote. “Simba waliniacha zikiwa zimebaki saa mbili kabla ya dirisha la usajili kufungwa na nilishakata tamaa kuendelea kucheza Tanzania ila bahati nzuri Yanga wakanisajili kwa muda huo.



“Niliondoka na nilikuwa nawadai fedha nyingi sana, kama ndiyo ningekuwa nimeondoka naamini wasingenipa haki yangu, lakini nilitafuta mwanasheria palepale Tanzania na mwingine alikuwa Mkenya anayefanya kazi Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa). “Kiukweli walinisaidia kwa sababu baada ya kwenda TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na mwanasheria wangu, nikapata haki yangu ambayo ilikuwa inapotea kama nisingeifuatilia
vizuri.


Tambwe akiwa na rafi ki yake pamoja na mkewe.

UTAKUMBUKA NINI YANGA BAADA YA KUONDOKA?

“Yapo mambo mengi ambayo nitayakumbuka ila kubwa ni upendo wa kutoka kwa viongozi, hawakuwa wanabagua watu kwa madaraja kama ilivyokuwa ikielezwa mara nyingi. Kulikuwa na madai ulikuwa unafunga mabao kwa kutumia ushirikina, unasemaje?



“Unajua huwezi kumzuia binadamu kuongea kwa sababu kila mtu anasema lake, lakini mafanikio yangu ya kufunga mabao mengi yametokana na uwezo wangu binafsi. “Kinachonishangaza ni kwamba waliokuwa wakidai hivyo sina uhakika kama walikuwa watu wa mpira kwa kuwa huwezi kutumia huo ushirikina ukaweza kufunga mabao zaidi ya 70 ndani ya miaka sita. Ulicheza Yanga kipindi ambacho kulikuwa na uhakika wa fedha lakini hamkufi ka mbali kimataifa, tatizo lilikuwa nini?



“Nadhani watu wengi hawajui juu ya mpira wa Afrika kwa sababu wakati ule kweli tulikuwa na kila kitu lakini je tulikuwa tunacheza na klabu zipi? “Nakumbuka tulikuwa tunacheza na timu kubwa zilizo juu yetu ndiyo maana hatukuwa tukifanya vizuri sana.



BEKI YUPI KWAKO ALIKUWA KIKWAZO?

“Unajua shida ya mabeki wa Tanzania wengi wanatumia sana nguvu, sasa nilikuwa nawazidi kwenye eneo hilo, lakini mtu kama Aggrey Moris na Kelvin Yondani wapo tofauti, ila wengine wamekosa maarifa. “Nakumbuka nilishawahi kukabwa hadi nikatoka damu na yule beki wa Ruvu Shooting, George Michael na hiyo ilitokana na yeye kukosa akili, zaidi akawa anatumia nguvu, lakini bado niliweza kufunga.



UNA MPANGO SIKU MOJA KURUDI YANGA KAMA KOCHA?

“Kwanza kitu kama hicho sitaki hata kukisikia kwa sababu mimi nina hasira halafu ninajijua nilivyo na suala la kuwa kocha kwangu halipo ila nadhani siku moja naweza kuwekeza katika nchi hizi mbili, Burundi na Tanzania. HAPA

BURUNDI NJE YA SOKA UMEWEKEZA KWENYE NINI?

“Namshukuru Mungu, kiukweli nimewekeza kwenye kilimo, unajua hapa tunalima mihogo, mahindi na maharage, kwa Tanzania kule nalima mchele, hivyo inanisaidia kuendesha mambo yangu. UNAHISI SIMBA NA YANGA

ZINAKWAMA WAPI?

“Kitu kikikubwa ambacho nakiona kuanzia kwa wachezaji ile ya kuwaambia wamezeeka kwa kuwa wamecheza misimu mitatu au minne, hilo jambo kiukweli limekuwa ni kero kubwa. “Huwezi kumuona mchezaji mzee kwa kuwa amekosea siku moja, unapaswa kujua nini amefanya mwanzo, sasa katika hizi timu mbili hili jambo limekuwa kero na linakwamisha mambo mengi kwenye mpira. “Naamini kama viongozi wataachana nalo basi soka la Tanzania litabadilika kwa asilimia kubwa kwa sababu litatoa nafasi kwa wachezaji kuonyesha vipaji vyao ila kama hila na chuki zitaendelea hakuna kitakachofanyika.

UMEOA TANZANIA NA UNA MTOTO WA KIUME, UNATAMANI AJE KUWA NANI?

“Nataka aje kuwa kama mimi kwa sababu mtoto wa nyoka ni nyoka na kwa upande wa mtoto wangu anapenda sana mpira, kila siku anapasua mpira. “Lakini huko mbele ikitokea anataka acheze katika klabu za Tanzania basi
ningependa akacheze Yanga na siyo Simba kwa sababu naamini litakuwa ni jambo zuri. “Sasa hivi ninachoangalia ni yeye kuweza kupata malezi bora ikiwezekana kumpeleka kwenye akademi za nje kama Marekani au Uingereza kwa kuwa nina ndugu zangu wengi huko.



MTOTO WAKO AMEZALIWA TANZANIA VIPI KWA TIMU YA TAIFA? “Hilo halina ubishi, atacheza Burundi kwa sababu mimi baba yake ni Mrundi na huyu ni mtoto wangu hatoweza kucheza Tanzania licha ya kuwa nimeoa Tanzania.

“Sikatai kwamba amezaliwa Tanzania na siyo kwamba naichukia kwa sababu nitaendelea kwenda Tanzania kwa kuwa nina wakwe zangu na rafi ki wengi ambao nimeishi nao vizuri kwa kipindi cha miaka sita.

“Unajua Tanzania imenifundisha mambo mengi na Watanzania ni watu wazuri, wakarimu, wanyenyekevu na hawana shida kabisa kwa sababu siyo watu wa kufuatilia mambo ya mtu mwingine ambaye ametulia.



UNAKWENDA KUCHEZA LIGI YENYE USHINDANI ZAIDI NA WEWE UMEACHWA NA YANGA KWA MADAI KWAMBA UMECHOKA, UMEJIPANGAJE? “Mimi sijachoka, bado nipo fi ti kwa kuendelea kucheza lakini naweza kusema kwamba mfumo wa soka la Tanzania ndiyo ulikuwa umenichoka, huwezi kumuona mchezaji mzuri akiwa hapati mechi nyingi za kucheza.

“Ninapokwenda yupo Mbuyu Twite na wakati anaondoka aliambiwa amechoka, lakini mbona bado anacheza kwenye ligi ya ushindani hadi leo? Nimejipanga kwenda kufanya vizuri huko, bado sijachoka.



BAO GANI KATIKA LIGI YA BONGO LITABAKI KWENYE KUMBUKUMBU ZAKO? “Nimefunga mabao mengi muhimu lakini na mengine nimeshayasahu lakini ninachokumbuka ni kuweza kufunga mabao 76 ndani ya miaka sita niliocheza Tanzania, haikuwa jambo dogo.

MKEO NI MTANZANIA, UMEPANGA KUMRUDISHA BONGO KWA KIPINDI HIKI AMBACHO UNAKWENDA OMAN? “Arudi Tanzania kufuata nini, hawezi kurejea huko hata iweje, naondoka lakini yeye atabaki na familia hapa kwa sababu siwezi kwenda naye huko,” anasema Tambwe.