Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, amesema alama anayotaka kuiacha katika wilaya hiyo siku akiondoka ni kupaisha kiwango cha elimu.

Ndivyo pia anavyotaka akumbukwe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mussa Gama. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timu ya waandishi wa habari, viongozi hao wawili wamekiri kwamba hali ya elimu katika wilaya hiyo haikuwa nzuri miaka michache iliyopita kwa maana ya watoto wengi kutofaulu vizuri.

Jokate alisema kutokana na hali hiyo walichukua hatua ya kuanzisha kampeni ya ‘Tokomeza Zero Kisarawe aliyosema imezaa matunda kwa kuwa wanafunzi wameanza kufanya vizuri.

"Wakati sisi tulijielekeza katika kutokomeza (daraja) sifuri, watoto wameipokea vizuri na sasa wamekuja na kauli mbiu ya kupata ," alisema.

Alisema, katika muktadha huo wa kupaisha elimu Kisarawe, wamefanikiwa kuongeza shule mbili mpya kwa ajili ya kidato cha tano na sita na hivyo kuwa shule tatu, moja ikiwa ni shule kongwe ya Minaki.

Alisema mbali na ukarabati mkubwa wa miundombinu katika mashule ambao wamefanya na wanaendelea kufanya, wanatarajia pia kuongeza shule zingine mbili za kidato cha tano na sita.

"Lakini lingine tunakwenda kuanzisha shule ya sekondari ya bweni kwa ajili ya wasichana pekee," alisema na kuongeza kwamba anaamini shule hiyo itasaidia kuhamasisha wasichana wilayani humo kusoma.