SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), imejitosa kwenye sakata la staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ la kujitoa Wasafi.

Tangu Harmonize au Harmo aandike barua ya kujitoa kwenye lebo hiyo iliyomkuza kimuziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumekuwa na mitazamo tofauti kutoka kwenye makundi na watu binafsi nchini.

HARMO NA JPM

Mapema wiki hii, Harmo alifanya shoo ya heshima mbele ya Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Kiwanda cha Super Doll kilichopo Vingunguti jijini Dar na kupewa pongezi na mkuu huyo wa nchi.

Baada ya shoo hiyo, ili kuonesha anafuatilia mambo yanayojiri kwenye muziki, JPM alimtania Harmo kwa nini amejitoa Wasafi, lakini jamaa huyo hakuwa na nafasi ya kumjibu.


SERIKALI IMECHUKUA HATUA GANI?

Ili kujua kama kuna hatua zozote Serikali imechukua juu ya sakata hilo, Risasi Jumamosi lilimtafuta Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe, lakini jitihada ziligonga mwamba.

KATIBU MTENDAJI BASATA

Hata hivyo, jitihada hizo hazikuishia hapo bali zilihamia kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambayo ipo chini ya wizara hiyo na ndiyo inayoshughulika na wasanii, Godfrey Mngereza ambaye alitoa kauli ya Serikali juu ya sakata hilo.

“Kwa kifupi tu ni kwamba sisi kama baraza hatujapata barua rasmi kutoka upande wowote ule. Si Wasafi Company wala mwanamuziki Harmonize.

“Kwa hiyo kimsingi sakata hilo halijaletwa baraza la sanaa rasmi. “Kama likifikishwa kwenye baraza siwezi nikasema tutachukua hatua gani kwa sababu baraza la sanaa ni mzazi, ni mlezi, ni msajili wa wasanii wakiwepo vyama, mashirikisho, vikundi na msanii mmojammoja.

“Kwa hiyo ni jukumu letu kabisa, tukiletewa masuala kama la Harmonize tutakaa nao na kujaribu kusuluhisha kwa sababu migogoro wakati mwingine inatokea, lakini tuna wajibu wa kuweza kukalisha pande zote mbili na kuweza kuyazungumza.


LIKIFIKA LITASULUHISHWA

“Hakuna kitu ambacho kinashindikana kwani ndiyo jukumu mojawapo la baraza la sanaa, kutoa ushauri wa kiufundi kwa wasanii wetu na kushauriana nao kwamba migogoro haijengi.

“Tukiletewa suala hilo tutajaribu kusuluhisha kwa sababu migogoro wakati mwingine inatokea, lakini tuna wajibu wa kuwakalisha chini na kuzungumza kwani hakuna kitu ambacho kinashindikana.

MIGOGORO HAIJENGI

“Migogoro mara nyingi inarudisha nyuma maendeleo ya msanii mmojammoja au vikundi. Kwa hiyo mara nyingi tunafanya kila linalowezekana katika kutatua migogo pale inapojitokeza,” alisema katibu huyo mtendaji wa Basata.

Kwa maelezo hayo ni kwamba Basata wapo tayari kulishughulikia suala hilo kwani ni sehemu ya majukumu yake hivyo ni kiasi cha wahusika kulipelekea suala hilo kwenye chombo hicho.

HARMONIZE NA WASAFI

Harmo alianza rasmi muziki mwaka 2015 baada ya kusainiwa na lebo hiyo ya Mondi ambapo alisimamiwa kazi zake za muziki ikiwemo shoo za ndani na nje ya nchi, video, kolabo za kitaifa na kimataifa na mikataba mbalimbali.

Baadaye taarifa zilianza kusambaa kuwa Harmo baada ya kupata mafanikio ya ndani na nje ya nchi alianza kuona ana uwezo wa kujitegemea kwa shoo na pesa hivyo kuamua kwenda kujitegemea. Harmo amekuwa akijaribu kuzima maneno mengi ili isije ikaonekana ana bifu na Mondi. Hata hivyo, Mondi alikaririwa akisema kwa kifupi; “Kama Harmonize anataka kuondoka, aondoke.”