Saudi Arabia imeonyesha mabaki yaliyoteketea ya kile ilichosema ni makombora ya angani na ndege zisizokuwa na rubani zilizotumika kushambulia miundo mbinu yake ya mafuta.

Nchi hiyo ya kifalme imesema jumla ya makombora 25 yalirushwa katika visima vyake viwili vya mafuta. Msemaji wa Wizara ya ulinzi nchini humo Turki al-Malki amesema silaha hizo zilizopatikana zinajumuisha makombora ya Iran.

Al-Malki amewaambia waandishi wa habari kwamba mashambulizi hayo yalidhaminiwa na Iran.

 Mashambulizi hayo yalisababisha kupungua pakubwa kwa kiwango cha uzalishaji mafuta cha Saudi Arabia na waasi wa Houthi nchini Yemen wanaoungwa mkono na Iran na ambao wanapambana na majeshi ya muungano yanayoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen walikiri kuhusika.

 Msemaji huyo lakini amesema kuwa waasi hao walisema hivyo ili kuiondolea lawama Iran.