TANGU kuondoka kwa mwanamuziki Rajab Abdul ‘Harmonize’ kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) kuna harakati za ndani zinazofanywa kumpaisha memba mwingine wa kundi hilo, Raymond Mwakyusa ‘R ayvanny’.


Habari za chini ya kapeti zilieleza kuwa, mwaka huu wa 2019 huenda ukamalizika kwa mafanikio makubwa kwa Rayvanny kutokana na ‘fujo’ zinazofanyika za kumpaisha kimataifa.

Ilielezwa kuwa, kasi yake ya kufanya kolabo za kimataifa ni kubwa kama aliyokuwa nayo Harmonize au Harmo alipokuwa ndani ya lebo hiyo.Mpaka sasa Rayvanny ameshafanya kolabo na wanamuziki wakubwa duniani kama Pitbull, Jason Derulo na Nora Fatehi.

Habari nyingine nzito ni kwamba kwa sasa Rayvanny yupo kwenye maandalizi ya kolabo na mwanamuziki aliyewahi kufanya kazi chini ya lebo ya rapa mkubwa duniani, Jay-Z kupitia lebo yake ya Roc Nation anayefahamika kwa jina la Philly Freeway.


Kwa mujibu wa prodyuza maarufu wa Bongo Fleva, S2kizzy, Rayvanny na jamaa huyo tayari wameingia studio nchini Marekani na mwanamuziki mwingine anayefanya vizuri nchini Netherlands aitwaye Frenna.

Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta Rayvanny ambapo liliambiwa kuwa yupo nchini Marekani hivyo jitihada za kumpata zinaendelea.Hivi karibuni kuliibuka tetesi nyingi baada ya Harmo kusepa Wasafi ambapo watu wa karibu walidai kuwa Rayvanny ndiye anaandaliwa kuchukua mikoba ya jamaa huyo ambaye ameanzisha lebo yake ya Konde Gang.