Rais wa shirikisho la vyama vya wafanya kazi Tanzania TUCTA ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU bw.Tumaini Nyamhokya,amesema ni haki ya mfanyakazi kustaafu kwa hiari hivyo shirikisho halina tamko kwa wafanya kazi kutokana na habari zilizoenea mitandaoni kuwa watumishi wengi wameanza kuomba kustaafu kwa kuhofia KIKOKOTOO.

Rais wa TUCTA ameyasema hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU mkoa wa Njombe ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili ukiambatana na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

“Nimeulizwa na waandishi wa habari wengi kwamba watumishi wanastaafu kwa hiari wanakuwa na hofu,kustaafu kwa hiari kupo kwa mujibu wa sheria,mtu akiona atumie kustaafu kwa hiari ili apate fedha afanye mambo yake mengine hilo ni jambo jingine,na kama kuna mtu ameamua kustaafu kwa hiari ili asifike kule ambako kuna sintofahamu kwamba kuna KIKOKOTOO gani kitafuatia hiyo pia ni haki yake kwa mujibu wa sheria”alisema Nyamhokya

Nyamhokya ameongeza kuwa shirikisho hilo halina tamko la kuwaondoa hofu wafanyakazi.

“Kwa hiyo sisi hatuna tamko lolote la kuwaambia wafanyakazi,hatuna tamko lolote la kuwaondoa hofu,hofu ilikuwepo kubwa sana wakati kikokotoo kimebadilika na kikaja  kikokotoo ambacho kiukweli tunakiita kikokotoo kandamizi katika masalahi ya wafanyakazi hasa wale ambao wamekuwa wamestaafu sasa tumerejeshewa kiu na tumepewa muda wa miaka mitano tuweze kusimamia na kuandaa kwa hiyo timu zipo na zinaendelea kufanya kazi kuhakikisha tunaandaa kikokotoo ambacho kitakuwa rafiki kwa pande zote Mbili”aliongeza Nyamhokya

Katika hatua nyingine Nyamhokya amesema bado kuna badhi ya viongozi wa serikali na wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya kazi za kimihemko na kuwaumiza watendaji hali ambayo inasababisha kuvunjika moyo kiutendaji.

“Sehemu kubwa viongozi wanakwenda vizuri lakini kuna baadhi ya wanasiasa ambao ni wateule wa mheshimiwa Rais, sisi kama viongozi wa vyama tunaona hawatendi vyema,baadhi tumeona wana hulka ya kuchukua hatua zinaonekana kuwa za kinidhamu kwenye majukwaa,utaona wanatamka simtaki mtumishi huyu mkoani kwangu,au wanasema kuanzia sasa wewe sio mkuu wa idara kiukweli inaumiza sana”alisema Nyamhokya