Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ameweka wazi msimamo wake wa kuunda tume maalumu itakayopitia upya mradi wa Chalinze Mboga baada ya kuukuta na mapungufu mengi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri huyo kutembelea mradi huo na kubaini mapungufu katika utekelezaji wake ikiwemo udanganyifu wa vipimo vya ulazaji mabomba.

Mradi wa Chalinze Mboga ulianza Aprili mwaka huu ukiwa chini ya mkandarasi kutoka kampuni ya Shanx aliyekabidhiwa mradi huo na Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA).

Akitoa maamuzi hayo, Mbarawa amesema kampuni ya Shanx wamwfanya udanganyifu wa vipimo vya ulazaji wa bomba pamoja na kutaka nyongeza ya gharama kulingana na kiwango cha mawe alichokuta kwenye eneo la mradi.

Mbarawa amesema, amefikia maamuzi ya kuunda tume maalaum ili kuweza kupitia upya mradi huo ikiwemo na kuwaita Dawasa na Shanx ofini kwake ili kupitia upya 
maombi ya mkandarasi huyo.

"Ntawaita ofisini kwangu Dawasa pamoja na Mkandarasi ili kuweza kupitia maombi yao juu ya ongezeko la gharama za uchimbaji na ulazaji bomba, pia ntaunda tume maalumu itakayopitia upya mradi wa Chalinze Mboga," amesema Mbarawa.

Amesema, makubaliano ya awali ni kuchimba mtaro wa kulaza mabomba mita 1.8 ila wao wamechimba mita 1.6 kwenda chini tofauti na makubaliano yaliopo kwenye mkataba.

"Katika mkataba makubaliano ilikuwa kuchimba mita 1.8 kwenda chini na wanalipwa kulingana na kipimo cha uchimbaji ila kulingana na wanavyochimba ina maana malipo yao sio sahihi," amesema 

Mbarawa ameeleza kuwa Mradi huo unaenda vizuri lakini kuna mapungufu ikiwemo upande wa gharama za utandikaji bomba zina utofauti mkubwa sana ukilinganisha na mahala pengine.

Ameeleza kuwa mkandarasi wa mradi huo gharama zake za uchimbaji zipo juu ambapo anapima mita 1 kwa shilingi 49,000 wakati Arusha ni shilingi 32,000 kwa mita na wanachimba mita 2 kwenda chini. 

Mbarawa ameendelea na kusema kuwa, mkandarasi ameandika maombi ya ongezeko la gharama za uchimbaji na ulazaji bomba kulingana na kiwango cha mawe alichokuta kwenye eneo la mradi.

“Mkandarasi ameandika maombi ya ongezeko la gharama ya uchimbaji na ulazaji wa mabomba kutokana na kiwango cha mawe alichokikuta, jambo haliwezekani kwani atuwezi kuingiza pesa ya serikali kwa namna hii kilichobaki ni kuwatafuta wataalam ili waupitie upya," 

Mbarawa amesema, watalaamu hai watapitia “item by item” na kufahamu malipo anayelipwa Shanx ni sahihi na amedai kuwa kama wangemlipa malipo ya 32,000 kwa mita kazi ingefanyika.

Mbarawa amewataka Mamlaka ya Dawasa kusimamia vizuri mradi huo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaendana na mradi.

Mradi wa Chalinze Mboga utahudumia wananchi wa Maeneo ya Ruvu darajani, Vigwaza,Ranchi ya Taifa Ruvu (NARCO), Chahua -Lukenge, Visenzi, Buyuni na Mdaula -Unebazomozi. Kwingine ni Chamakweza, Pingi, Pera, Chalinze, Chalinze Mzee, Msoga na Mboga aidha, viwanda vitakavyofaidika ni pamoja na Twyford, kiwanda cha ngozi, kiwanda cha Matunda cha Sayona pamoja na watumiaji wengine wakubwa ikiwemo kampuni Yapi Merkezi wajenzireli ya kisasa (SGR).

Na Katika usanifu wa mradi huo, umetilia maanani ongezeko la watu na mahitaji ya miaka 20 ijayo na kutosheleza idadi ya watu hadi kufikia 120,912 ndani ya eneo la mradi na utakuwa kwa umbali wa Kilomita 58 ujenzi wa vituo viwili vya kusukumia maji na utagharimu bilion 14 hadi kukamilika kwake.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa akizungumza na mkandarasi wa kampuni ya Shanx baada ya kutembelea mradi wa Chalinze Mboga na kukuta mapungufu mengi ikiwemo udanganyifu wa vipimo vya ulazaji mabomba na ongezeko la gharama za uchimbaji wa mtaro huo.

Mkandarasi akiwa anaendelea na kazi yake ya uchimbaji mtaro wa kulaza mabomba.