Ndege ya Air Tanzania imetua nyumbani Tanzania mwendo wa saa mbili unusu usiku huu baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya Afrika Kusini.

Shirika la ndege hiyo imeandika katika ukurasa wake wa Tweeter kuwa safari za ndege hiyo kuelekea Afrika kusini zitarejea siku ya ijumaa.


Mapema jana Mahakama Kuu ya jimbo la Gauteng imeamuru ndege ya Air Tanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini kuachiwa mara moja.

Mwandishi wetu wa Afrika Kusini Nomsa Maseko anasema kuwa utaratibu wa kuiachia ndege hiyo kurejea Dar es Salaam kutoka uwanja wa ndege wa OR Tambo jijini Johannesburg unaendelea.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Dkt Damas Ndumbaro aliyekuwepo mahakamani ameileza BBC kuwa Tanzania imeridhishwa na uamuzi wa mahakama.

Mkulima ambaye alipeleka shauri hilo mahakamani Hermanus Steyn na kupata kibali cha kushikiliwa ndege hiyo, hakuridhishwa na hukumu ya awali na kukata rufaa.

Mwandishi wa BBC Maseko anaripoti kuwa Bw Steyn amedondoshwa pia kwenye rufaa yake na kutupiliwa mbali na mahakama.


Jaji Twala M L akisoma hukumu yake mapema jana kuamuru ndege ya Tanzania kuachiwa
Dkt Ndumbaro ambaye pia ni wakili amesema kama Steyn bado ana madai yeyote, inafaa arudi kwenye mahakama za Tanzania na kusikilizwa.

"Oh, niamini, raisi (John Magufuli) tayari ameshapewa taarifa (ya hukumu)," mwandishi wa BBC aliyepo mahakamani anamnukuu Dkt Ndumbaro akisema.