MTOTO mzuri wa sura na sauti Bongo, Faustina Charles ‘Nandy’ anafanya vizuri kiasi cha kufanana na anayoyafanya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Kwa siku za hivi karibuni, mrembo huyo amekuwa akijaza uwanja na kufanya shoo ambazo zimetajwa kumuumiza kichwa Diamond na kruu nzima ya Wasafi Classic Baby (WCB).

“Nandy anamkaba koo Mondi yani ni bampa to bampa. Yaani Diamond na Wasafi wakipiga shoo na kujaza uwanja, Nandy naye anafunga uwanja vya kutosha,” kilisema chanzo na kuongeza:

“Habari wanayo wakazi wa Kahama, Sumbawanga, Tanga na Bukoba ambako kote huko Nandy ameacha vumbi la hatari.”

Chanzo hicho kilicho karibu na WCB kimepenyeza ubuyu kuwa, kitendo cha mrembo huyo kufanya shoo zake maarufu kwa jina la Nandy Festival kinauumiza sana kichwa uongozi wa WCB ambao unatamani kumsajili staa mwingine wa kike, Ruby ili aweze wamdhibiti Nandy.

“Nasikia uongozi unalitajataja sana jina la Ruby (Hellen George) kama mtu ambaye wanaweza kumsajili ili wamzidi kete Nandy,” kilisema.

Kuhusu madai hayo, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na Rubby ili kutaka kujua kama WCB wameshamfikia au kufanya nao mazungumzo ya kikazi ambapo alijibu kwa kifupi:

“Hayo mambo unatakiwa uulizwe uongozi wa WCB ndio una majibu kamili.”

Jitihada za kuupata uongozi wa WCB hazikuzaa matunda baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.Alipotafutwa Nandy na kutaka atoe maoni yake kuhusiana na yeye kuwatikisa Wasafi kiasi cha uongozi kudaiwa kuwa upo mbioni kumsajili Ruby ili kumwangamiza, alishtushwa na habari hiyo.

“(Anacheka sana) Heeh! Yaani huwezi amini ndio napata hizi taarifa toka kwako, unajua WCB nawaheshimu sana kama ndugu zangu kwa sababu mara kadhaa tumekuwa tukishirikiana vizuri kwenye kazi, hivyo sidhani kama kweli wanaweza kuwa na mpango wa kunizuia kwa namna yoyote,” alisema mrembo huyo ambaye anatamba na wimbo wa Hallelujah aliofanya na Willy Paul wa Kenya.Alipoulizwa kuhusu siri ya mafanikio yake, Nandy alisema:

“Mimi namwamini Mungu maana ndiye aliyenifikisha hapa nilipo, naamini ndio siri ya mafanikio na hakuna mwanadamu yeyote atakayeweza kunishusha.