Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Geita mjini, Mhe.Constantine Kanyasu amewahimiza wazazi wenye watoto waliomaliza darasa la saba mwezi huu nchini  wahakikishe wanawalinda watoto hao wasijiingize katika makundi yasiyofaa.

Akizungumza kwenye mahafali ya saba ya wanafunzi 69 waliomaliza darasa la saba katika shule ya msingi ya Waja Springs ya mkoani Geita,Mhe.Kanyasu amewataka wazazi wawe mstari wa mbele katika malezi bora ya watoto wao

.Aidha, Mhe.Kanyasu amewataka pia wahitimu hao wakawe mfano bora katika jamii kwa kuwa kuwasaidia wazazi wao kwa kufanya kazi za majumbani badala ya kuacha kazi zote zifanywe na Wafanyakazi wa ndani

Katika hatua nyingine, Mhe. Kanyasu ameipongeza shule hiyo kwa kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa na  kuufanya mkoa wa Geita kuwa miongoni mwa  mkoa inayokuwepo kwenye tano bora kitaifa.

Pia, Mhe.Kanyasu amewataka wanafunzi hao watumie muda mwingi kujisomea vitabu vya hadithi badala ya kutumia muda mwingi kuangalia Televisheni hasa vipindi visivyofaa

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameuhakikishia Uongozi wa shule hiyo kutafuta ufumbuzi wa tatizo la barabara iinayoelekea katika shule hiyo pamoja tatizo maji machafu wakati mvua ikinyesha .

Kwa upande wake Meneja wa Shule hiyo, Mhandisi.Chacha Wambura amewaasa wazazi kujiepusha kuwapatia simu watoto wao ili wasiweze kuingia katika vishawishi katika kipindi hili kifupi walichohitimu masomo yao.

" Wazazi jiepusheni kuwapa simu zenu hawa watoto, hii mitandao ya kijamii inawapelekea watoto kuanza kuangalia mambo yasiyofaa " alisisitiza Wambura.

Aidha, Amewataka Wahitimu hao waache kuzitumia simu za wazazi wao pindi wakiwa majumbani badala yake wasome vitabu kama walivyokuwa wakifundishwa shuleni

Naye, Janeth Ndibalema ambaye ni mzazi wa mhitimu wa darasa la saba, Amesema malezi ya watoto kwa sasa yamekuwa na changamoto nyingi kutokana na wazazi kuacha jukumu la malezi kwa Wasichana wa kazi  hali  inatopelekea watoto wengi kuharibikiwa.

Kufuatia hali hiyo, Ndibalema ametoa wito kwa wazazi kutenga muda kukaa na watoto wao badala ya kujikita kwenye majukumu ya kazi ili kuwasaidia watoto wao kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa yatakayowafanya wasiweze kuendelea na shule.