Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Jophn Wanga, akipokea cheti cha uchangiaji wa damu kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio (kushoto) jana.

WADAU na Wataalamu wa afya wametakiwa kuweka mkakati wa kuelimisha na kuhamasisha jamii kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya watu.

Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio, wakati akiwakabidhi vyeti wadau waliofanikisha uchangiaji damu kwenye maadhimisho ya siku ya damu yaliyofanyika mkoani Mwanza kitaifa , Juni mwaka huu.

Alisema ili kuokoa maisha ya wananchi wenye uhitaji wa damu wadau na wataalamu wa afya waweke mkakati endelevu wa kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha uchangiaji damu.

“Wataalamu wa afya mnatakiwa kulifanya zoezi la uchangiaji damu kuwa endelevu na hivyo mtafute jukwaa la kuelimisha jamii ili tufike mahali ijenge utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari na kuweza kutatua changamoto hiyo,”alisema Kadio.

Pia alishauri kutokana na hospitali nyingi kumilikiwa na taasisi za dini ni vyema viongozi wa madhehebu ya dini wakawahamasisha waumini wao kuona umuhimu wa kutoa damu kwa maslahi ya jamii.

Awali Mkuu wa Huduma Maabara Mkoa wa Mwanza, Julius Shigela alisema wadau hao wametunukiwa vyeti hivyo ili kutambua na kuthamini mchango wao kutokana na mafanikio ya ukusanyaji na uchangaji damu.

Alisema Mkoa wa Mwanza katika maadhimisho ya damu duniani yaliyofanyika jijini humu Juni mwaka huu, ulifanikiwa kukusanya unit (chupa) 10,669 na kuvuka lengo la wizara kwa asilimia 203, kwa mkoa wakivuka kwa asilimia 101 la kukusanya chupa 4000.

Miongoni mwa wadau waliotunukiwa vyeti kwa niaba yaw engine  zaidi ya 30 ni pamoja na The Desk & Chair Foundation,halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, Isamilo Lodge,Aga Khan Foundation, hospitali za Pasiansi SDA,Hindu na CF. 
Michael Mugerwa, Meneja mradi wa IMPACT wa Aga Khan Health Service akipokea cheti kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio kwa kutambua mchango wa taasisi hiyo katika uchangiaji damu jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio (kushoto) akimtunuku cheti mdau mkubwa wa uhamasishaji wa uchangiaji damu, Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Alhaji Sibtain Meghjee, hafla iliyofanyika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza jana.
Meneja Masoko wa Isamilo Lodge Grace Kakwezi akipokea cheti cha kutambua mchango wa hoteli hiyo katika ushiriki wake wa kuchangia damu kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Christopher Kadio (kushoto) jana.
Dk. Mabuba wa Hospitali ya SDA Pasiansi (kulia) akipokea cheti kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio jana baada ya hospitali hiyo kushiriki zoezi la uchangiaji damu.
Mdau wa uhamasishaji wa uchagiaji dau aliyefahamika kwa jina moja la Peter akiaokea cheti cha kutambua mchango wake kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio jana.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Wanga,akipokea cheti cha uchangiaji damu kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba, jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio akizungumza na wadau na wataalamu wa afya kwenye kikao kazi muda mfupi baada ya kuwatunuku vyeti wadau wa uhamasishaji wa uchangiaji damju waliofanikisha zoezi hilo Juni mwaka huu kwa kukusanya chupa 10,669. Picha na Baltazar Mashaka