Aliyekuwa  Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Septemba 17, 2019, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dilunga alilazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Septemba 9, mwaka huu akitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa rufaa kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo.

Madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamejitahidi kwa kila hali, ila Mungu amempenda zaidi.

Kampuni ya Jamhuri Media Limited kwa kushirikiana na familia ya Dilunga tunaandaa taratibu za kuaga mwili hapa jijini Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika Morogoro alikozaliwa katika siku itakayotangazwa na familia.

Mwili utasafirishwa kwenda Morogoro kesho Septemba 18, 2019. Msiba uko Kimara Stopover kwa dada.

Dilunga ameajiriwa JML tangu Februari 1, 2019 kama Mhariri wa Gazeti la JAMHURI, ambako amefanya kazi hadi mauti yalipomfika.

Kabla ya kujiunga JAMHURI, Dilunga amepata kufanya kazi na Gazeti la Raia Mwema na Mtanzania miaka ya nyuma.

Kwa muda mfupi aliofanya kazi Gazeti la JAMHURI, Dilunga amekuwa mtu wa msaada na ametoa mchango mkubwa katika kuboresha maudhui ya gazeti hili la Uchunguzi. Hakika pengo lake ni vigumu kuzibika. Tunasikitika sana.

Tunawashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mwananyamala na Muhimbili, wahariri, waandishi wa habari, maafisa uhusiano, wanasiasa na watu mbalimbali ambao wamefika Muhimbili kumjulia hali wakati wa ugonjwa wake na tunaomba tuuendeleze mshikamano tuliouonyesha katika kipindi hiki, sasa na baadaye.

Dilunga alizaliwa Oktoba 28, 1976. Ameacha mjane na watoto watatu. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.

Deodatus Balile
Mkurugenzi Mtendaji
Jamhuri Media Limited