Mtoto wa miezi mitano Jijini Dar es salaam, katika hospitali ya Muhimbili amekatwa kiganja cha mkono wake wa kushoto baada ya kupatiwa huduma za matibabu ya sindano kupitia mshipa wa mkononi na kupelekea mkono huo kuharibika na kukatwa kabisa.

Matibabu hayo alikuwa akifanyiwa katika hospitali ya Mwananyamala ambapo baadae alipewa rufaa katika hospitali ya Muhimbili baada ya kuona hali ya mtoto inazidi kuwa mbaya na mkono ukizidi kubadilika rangi na kuwa mweusi huku ukisinyaa.

Mama wa mtoto huyo alianza kuona mkono wa mtoto wake ukibadilika lakini mara baada ya kuripoti hali hiyo kwa madaktari hospitali ya Mwananyamala walisema kuwa damu imevilia hivyo walimshauri mama huyu kuchukua mkono wa mwanae na kuweka kwapani hadi utaporudi katika hali ya kawaida.

Mama huyo alieleza hayo pindi alipohojiwa na chombo cha habari cha TBC, na kusema kuwa chanzo kilichopelekea mtoto wake kufikia hatua hiyo ni kutokana na kanyula aliyowekewa siku chache zilizopita alipofika kufanyiwa matibabu baada ya kushikwa na homa kali.