Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Joyce Ndalichako (wapili kulia) na Askofu Thomas Skrenes (wapili kushoto) wakikata utepe wa uzinduzi wa jengo la kulelea watoto Yatima katika kanisa la KKKT Kimara. Wengine pichani ni Mchungaji wa Kanisa la KKKT Kimara Wilbroad Mastai (kushoto) na Askofu Msaidizi, Chadiel Lwiza (kulia).
Usharika wa K.K.K.T. – Kimara ambao ni sehemu ya Jimbo la Magharibi, Dayosisi ya Mashariki na Pwani umetimiza miaka 10 ya Baraka na Utumishi kwa kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa washarika wake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kuadhimisha miaka 10 tangu Mchungaji (Mch.) Wilbroad Mastai alipopewa dhamana ya kuwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kimara, Kanisa hilo limeweza kupitia mafundisho imara kuhusu uchumi Kibiblia kuwajengea maarifa washarika namna ya kumiliki na kutawala uchumi wao.
Taarifa hiyo pia imeongeza kuwa Kanisa limeweza kufungua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kwa shule ya awali na msingi inayotambulika kwa jina la Jerusalem Pre & Primary School na kununua shule ya Sekondari inayotambulika kwa jina la Bunju Boys.
Mafanikio mengine ni pamoja na kujenga kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo Usharikani hapo, kujenga Hospitali pitakayokuwa chini ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani na kumiliki hisa Mendeleo Benki.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mch. Mastai alisema: “Fadhili za huyu Mungu kwetu sisi hazihesabiki wala hazielezeki. Hata kwa vitu vya mwilini tu, ndani ya hii miaka kumi, Mungu ametuongeza na kutuzidisha.”
“Wapendwa tulioko hapa leo hii, sisi wa usharika wa Kimara tumetafakari, tumejipima na kujitathimini, tukajiridhisha kuwa katika kipindi cha muongo mzima, mimi pamoja na waumini wa usharika huu, tukimwabudu Mungu na kutumika hapa usharikani, tumepewa neema na upendeleo mwingi sana, kwa Baraka za Rohoni na za mwilini,”
Mch. Mastai aliongeza kuwa “Mungu ameyagusa maisha yetu kwa mtu mmoja mmoja na pia kama Usharika. Na hata watu wengine wengi tusiowajua na wale wasiotujua, walisikia habari za Mungu wetu anayerehemu, wakakimbilia mahali hapa. Wengi wana neno la kusema juu ya wema wa Bwana. Fadhili za huyu Mungu kwetu sisi hazihesabiki wala hazielezeki. Hata kwa vitu vya mwilini tu, ndani ya hii miaka kumi, Mungu ametuongeza na kutuzidisha.”
Mch. Mastai alitoa shukran kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi njema anayoendelea kuifanyia nchi ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanyika hapa nchini.
“Tunamshukuru, tunampongeza na kumtakia Baraka za Mungu Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kazi yake ni njema sana. Tanzania inajengwa na inajengeka. Tanzania inajua hilo, Dunia inatambua hilo, Kuzimu nayo inajua hilo, hata Mbingu za Mungu wetu kwa kuwa ndiko yatokapo mema yote.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga akitoa ujumbe kwa waumini walioshiriki ibada maalumu ya shukrani kwa baraka na utumishi katika kanisa la KKKT Kimara.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Joyce Ndalichako akiongea na waumini waliohudhuria ibada maalumu ya shukrani kwa baraka na utumishi katika kanisa la KKKT Kimara.
Mchungaji wa Kanisa la KKKT Kimara Wilbroad Mastai (aliyesimama) akifafanua jambo katika ibada maalum ya shukrani kwa baraka na utumishi katika kanisa hilo.
Mwalimu wa neno la Mungu Christoher Mwakasege akiongoza maombi kwa waumini walioshiriki ibada maalumu ya shukrani kwa baraka na utumishi katika kanisa la KKKT Kimara.
Washarika wa KKKT Kimara wakisikiliza mafundisho ya Mwalimu Christopher Mwakasege (hayupo pichani) alipohudhuria ibada maalumu ya baraka na utumishi kwa washarika wa Kimara.