Mahakama ya Ufaransa imetoa hukumu ikumuunga mkono mmiliki wa jogoo mmoja baada ya kelele za alfajiri za kuku huyo kuwakera majirani zake.

Maurice kutoka kisiwa cha Oleron katika pwani ya Atlantic alituhumiwa kwa kuwakera wanandoa waliostaafu wanaomiliki nyumba ya likizo katika eneo hilo.

Habari za matatizo yaliomkabili zilisambaa kote duniani na kupata mashabiki chungu nzima.

''Ni ushindi wa kila mtu aliyepo katika hali yangu .Natumai uamuzi huo utakuwa wa kuigwa'' , alinukuliwa na gazeti la AFP akisema.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo mwezi Julai, mawakili wake walikuwa wamehoji kwamba malalamishi hayo ni hafifu kwa kuwa kuwika kwa kuku huyo ni hali ya kawaida ya maisha ya taifa hilo.

Bi Fesseau ambaye aliishi katika kisiwa hicho cha Oleron kwa miaka 35 katika pwani ya Atlantic angelazimika kuondoka eneo hilo ama kumnyamazisha kuku wake iwapo jaji angetoa hukumu dhidi ya jogoo hilo.

Sasa atalipwa Yuro 1000 kama malipo ya kumpotezea wakati wake mawakili wake walisema siku ya Alhamisi.

Bi Fesseau alijaribu kumnyamazisha Maurice - ikiwemo kumuwekea nguo mdomoni
Kesi hiyo iliungwa mkono na watu 140,000 katika mitandao ya kijamii waliowasilisha ombi la kuipinga.

Jogoo mwenye umri wa miaka minne amekuwa maarufu nchini Ufaransa ambapo jogoo yupo katika nembo ya taifa.

Biashara zimefanya kwa niaba yake huku barua za kumuunga mkono zikitoka kutoka umbali wa Marekani kulingana chombo cha reuters.

Kesi hiyo iliopata umaarufu imezua wasiwasi mkubwa kati ya wakaazi wanaoishi mashambani nchini Ufaransa na wale wanaohamia mashambani ili kutoroka maisha ya mijini.

"Huu ndio uvumilivu - lazima ukubali mila za mitaani," Christophe Sueur, meya katika kijiji cha Bi Fesseau, aliiambia AFP.

Meya wa mji mwingine, Bruno Dionis du Sejour, aliandika katika barua ya wazi mnamo mwezi Mei akitaka kelele za maisha ya vijijini - ikiwemo zile za ng'ombe na kengele za kanisani - ziandikwe kwenye orodha ya urithi wa Ufaransa ili kuwalinda dhidi ya malalamishi kama hayo