Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.
JAJI Mstaafu wa Mahakama Kuu Tanzania, Mohamed Chande Othman amesema pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mawakili nchini wapatao 6750, bado watu wengi wa mikoani wamekuwa wakikosa uwakilishi wa mawakili wa kujitegemea huku wengi wakitajwa kujazana mijini.

Amesema kwa makadirio ya Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 58, wakili mmoja anahudumia watu 82,857 wakati Afrika Kusini ambao inalingana kwa kiasi kikubwa na idadi ya watu wakili mmoja anahudumia watu 2,500.

Jaji Chande ameyasema hayo wakati akitoa mhadhara (Lecture) wa Jukumu la wanasheria chipukizi kwa umma na mwelekeo wa sekta ya sheria Tanzania kwa wanasheria wachanga jijini Dar es Salaam walipokutana pamoja kujadiliana mambo mbali mbali ikiwemo kuhamasisha wanasheria wachanga ambao bado hawajasajiliwa na wale waliosajiliwa kufanya kazi kwa weledi.

Jaji Chande amewaambia wanasheria hao kuwa mawakili wanatakiwa kwenda kufanya kazi vijijini na kama maofisa wa mahakama wakasaidie katika utoaji haki na kuongeza kuwa, asilimia 70 za kesi nchini zipo Mahakama za Mwanzo lakini wananchi wanajiwakilisha wenyewe.

Amewaambia kuwa wakiwa kama wanasheria vijana wanapaswa kuhakikisha wanafikia wananchi waliopo vijijini ili kuwasaidia katika masuala yao ya kisheria na kusaidia mahakama katika utoaji haki kwa haraka zaidi kwani mawakili wengi wamekuwa wakiishia kufanya kazi mijini kuliko vijijini.

Pia amewataka kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuafuata maadili yao kwa kuwa wakweli na kuepuka vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanalinda utawala wa sheria na haki za msingi, uhuru na wajibu.

" Katika Mkoa wa Lindi, kuna wakili mmoja huku mawakili nane wakiwa katika Mkoa wa Katavi, 20 mkoani Ruvuma, 29 Kigoma na 38 wapo mkoani Mara.

Aidha Jaji Chande amesema kuna baadhi ya mikoa takribani saba ya Tanzania Bara haina Mahakama Kuu kama vile, Lindi, Katavi, Morogoro, Simiyu, Manyara, Pwani, Singida and Songwe huku Wilaya 28 zikiwa hazina Mahakama za Wilaya kama vile Mkinga.

"Kutokuwepo kwa mahakama ni kikwazo kikubwa katika utoaji wa haki na masuala ya sheria hususani kwa mawakili wachanga. Hivyo, tutaendelea kuishauri serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili watu waweze kupata haki zao natambua kuna mchakato wa mahakama wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na mahakama," amesema Jaji Chande.

Amefafanua kuwa katika ripoti ya dunia ya mwaka 2019 kuhusu utoaji haki inaonesha watu milioni 230 wanaoishi katika mazingira mbalimbali wanakosa haki huku watu bilioni 1.5 wanashindwa kutatua matatizo yanayowakabili yanayohusu haki na watu bilioni 4.5 wametengwa na fursa zitolewazo na sheria na inaonesha kutokuwepo kwa usawa au ufikishaji sawa wa haki kwa wote na ukosefu mkubwa wa uwakilishi wa kisheria.

Jaji Chande amesema katika miaka mitano iliyopita zaidi ya asilimia 50 ya mawakili wamepokelewa nchini kufanya kazi hivyo, anaamini wataendelea kubadilisha muundo na taasisi ya sheria.

Kwa upande wake Balozi Juma Mwapachu amesema serikali imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha miundombinu ya mahakama lakini bado watu wengi wana uhitaji wa kusaidiwa katika masuala ya utoaji haki.

"Wanasheria wachanga wanatakiwa kujua wanaisaidiaje jamii katika masuala ya sheria pamoja na kupigania haki za binadamu, uhuru wa kuongea na katiba" amesema.

Naye, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu (TDHRC), Onesmo Olengurumwa amesema ni wakati wa mawakili kuhakikisha wanakwenda vijijini kuwasaidia wananchi waliowengi ambao hawajui masuala ya sheria.

Amesema, wanasheria wanapaswa kuwa na wito na uelewa mkubwa katika kuendesha kesi zenye maslahi kwa umma na zile za ki mkakati zaidi.

Olengurumwa ameongeza kuwa, kwa sasa kuna changamoto kubwa kwa mawakili kurundikana mijini, kwani nchini kuna mawakili wapatao 8000 lakini nusu ya hao wako mijini hivyo wanapaswa kujua wameitwa katika kazi hivyo kusaidia watu wote.

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohammed Othman Chande akitoa Lecture kwa wanasheria wachanga kuhusu majukumu yao kwa jamii na taaluma hiyo wakati wa sherehe ya majadiliano baina ya wanafunzi hao iliyofanyika katika chuo cha sheria jijini Dar es Salaam.
Balozi Juma Mwapachu akizungumza na wanasheria wachanga wakati wa sherehe ya majadiliano baina ya wanafunzi wa sheria, iliyofanyika mijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu (TDHRC), Onesma Olengurumwa akizungumza wakati wa sherehe ya majadiliano baina ya wanafunzi hao iliyofanyika katika chuo cha sheria jijini Dar es Salaam.
Picha ya Pamoja
Naibu Mkuu wa Taasisi, Fedha na Utawala wa chuo cha sheria (TLS) William Pallangyo akimkabishi Balozi Mwapachu jarida la takwimu za sheria wakati wa sherehehiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.Picha ya Pamoja