Iran imesema Uingereza inapaswa kuacha kuiuzia silaha Saudi Arabia, badala ya kuishutumu Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Kauli hiyo imetolewa leo baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kusema kuwa nchi yake inaamini Iran imehusika na mashambulizi katika vituo vya mafuta vya Saudi Arabia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran, Abbas Mousavi amesema serikali ya Uingereza badala ya kuelekeza juhudi zisizozaa matunda dhidi ya Iran, inapaswa kuchukua hatua na kuacha kuuza silaha za maangamizi kwa Saudi Arabia, ambalo ni ombi la watu wengi duniani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, Mousavi ameitaka Uingereza kujiondoa katika madai ya uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Yemen.