Na Jumbe Ismailly, SINGIDA    

JESHI la Polisi Mkoani Singida na Uongozi wa Hopitali ya Rufaa ya Mkoa huo wameanza kutupiana mpira kutoa taarifa sahihi juu ya malalamiko ya baadhi ya ndugu wa marehemu, Amosi Mbua Muve wanaodai kuwa mwili wa ndugu yao ulinyofolewa baadhi ya viungo ukiwa umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali hiyo.

Katika tukio hilo lililotokea aug,26,mwaka huu saa mbili usiku, mmoja wa ndugu wa marehemu, Daudi Amosi Mbua mkazi wa Kitongoji cha Mwacheche, Kijiji cha Mtamaa “A” alisema baada ya baba yake kufariki muhudumu wa afya katika zahanati ya Kata ya Mwankoko ndiye aliyekwenda kuthibitisha kifo hicho.

Alifafanua kwamba baada ya taarifa za muhudumu huyo, wao kama familia walifanya makubaliano ya kuupeleka mwili wa marehemu baba yao kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Kwa mujibu wa Mbua, aug, 27 waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hadi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ukiwa na viungo vyake vyote kamili na kupokelewa na Daktari aliyekuwa zamu siku hiyo na baada ya kupatiwa nyaraka husika walimpeleka chumba cha kuhifadhia maiti ambapo muhudumu wa chumba hicho alimpokea akiwa na viungo vyote.
Baadhi ya ndugu,jamaa na marafiki wa marehemu AMOSI MBUA mkazi wa Kitongoji cha Mwachenche,Kijiji cha Mwankoko,Manispaa ya Singida ambaye mwili wake ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kukutwa ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo vyake.

“Baba yetu alipokelewa na muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti akiwa salama na viungo vyake vyote na tukapewa kibali cha maandishi kwa makubaliano kwamba aug,29, tutakapokuja kumchukua baba yetu tuje nacho na kulipia gharama zote za kuhifadhia mwili wa marehemu baba yetu.”alisisitiza mtoto mkubwa wa marehemu Amosi.

Alisema katika hali ya kushangaza aug,29 walipofika kuuchukua mwili wa marehemu baba yao muhudumu wa chumba hicho ndipo alimmwambia kuwa anasikitika kuwa kuna taarifa ambayo siyo nzuri ambayo hata yeye hajawahi kuiona tangu alipozaliwa.

Kutokana na taarifa hiyo hivyo alimshauri atafute wazee wawili au watatu ili wakashuhudie taarifa atakayokwenda kuambiwa, ushauri ambao aliutekeleza kwa kutafuta wazee wawili akafuatana nao na alipofika na kufunguliwa jokofu alilohifadhiwa marehemu baba yao na baada ya mwili kufunuliwa alishangazwa kuona baadhi ya viungo kukosekana.

“Tulipofika kwenye jokofu la kumhifadhi baba yangu alifungua kufuli lililokuwa limefungwa akavuta ile trei kumsogeza karibu ili tumuone ile tu anaonekana niliona paji la uso la baba limechunwa ngozi pamoja na nyama na ngozi ilikuwa imechunwa kuanzia kwenye paji la uso hadi robo tatu ya pua ilikuwa imechukuliwa haikuwepo na hata ngozi haikuonekana ilipo.”alisisitiza.
Hata hivyo mtoto huyo mkubwa wa marehemu alivitaja viungo vingine vilivyotoweka kuwa ni pamoja na mdomo wa juu,chuchu ya titi la kulia haikuwepo na ndipo walipoingiwa na mashaka kutokana na tukio hilo kutokuwa la kawaida na kuanza kuhojiana na muhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti ambaye naye alitupa maelekezo ya kwenda kuonana na Katibu wa afya wa Hospitali hiyo.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dkt. Deogratius Banuba licha ya kukiri kuwepo kwa tukio hilo lakini alikataa kuzungumzia chochote kuhusu hatua zilizochukuliwa au zinazotarajiwa kuchukuliwa kwa madai kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi zaidi.

 Walipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, ACP. Sweetbert Njewike pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo lakini akasema mwenye jukumu la kuongelea suala hilo ni Mganga mkuu wa Mkoa wa Singida na wala siyo jeshi la polisi.

“Kwa kweli taarifa za tukio hili ninazo lakini baada ya kuzipitia nimegundua kuwa anayetakiwa kulizungumzia tukio hili ni mganga mkuu wa mkoa kwani marehemu alikufa kifo cha kawaidi na kama angekuwa ameuawa au ni ajali ningehusika kikamilifu kulitolea maelezo.”alifafanua kamanda Njewike.

Akiongea kwa njia ya simu mganga mkuu wa mkoa wa Singida,Dkt,Victoriana Ludovic aliahidi kulizungumzia suala hilo leo (jana) kwa madai kwamba yupo Dodoma kwenye kikao hivyo mpaka apumzike na kulitafakari jambo hilo.