Hatima ya aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na wenzake inatarajia kujulikana Septemba 17, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo itatoa uamuzi kama wana kesi ya kujibu ama lah.

Hatua hiyo inatokana na Wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai kumueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wanafunga ushahidi wao baada ya kuleta mashahidi 10.

Baada ya Wakili Swai kudai wamefunga ushahidi wao, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, mwaka huu kwa ajili ya uamuzi, kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama lah.

Awali, Mtaalamu kutoka Maabara ya Uchunguzi Sayansi Jinai iliyopo makao Makuu ya Polisi, Faustine Mashauri (41) amedai mahakamani hapo kuwa saini zilizopo kwenye hundi ya benki ya CRDB pamoja na fomu za maombi ya kuhamisha fedha ni za Evans Aveva na Godfrey Nyange maarufu Kaburu.

Shahidi huyo wa tisa amedai kuwa amekuwa akifanya kazi ya kuchunguza vielelezo vinavyobishaniwa vilivyopo kwenye maandishi, saini na mihuli.

Akiongozwa na Swai, shahidi amedai wanatumia vifaa vya kielektroniki kuchunguza utata huo na kuwasaidia kuona tabia za uandishi kwa ubora na ukubwa wake.

Mashauri amedai Septemba 4,2017 alipokea bahasha iliyofungwa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Takukuru na ndani yake kulikuwa na nyaraka za hundi ya Benki ya CRDB na fomu ya maombi ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.

Alidai aliombwa kufanya uchunguzi wa kitaalamu kuhusu saini za Aveva na Nyange ili kujua kama kuna uwiano au utofauti.

“Nilibaini kwamba saini zilizokuwa kwenye hundi pamoja na saini walizoziweka wenyewe ambazo huzitumia kila siku zilikuwa zinafanana. Hii inamaanisha kwamba wale waliochukua fomu za kuhamisha fedha ndio waliosaini kwenye nyaraka zote,” alidai Mashauri.

Alidai baada ya uchunguzi aliandaa ripoti kuonesha alichokibaini katika uchunguzi wake na kurudisha Takukuru kwa hatua nyingine za kisheria.

Hata hivyo, shahidi aliomba mahakama kupokea ripoti hiyo kama kielelezo katika kesi hiyo na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zachariah Hans Pope.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 10 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba thamani ya Dola za Marekani 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.