KUFURU nyingine! Staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, kila kukicha ana habari mpya. Safari hii, jamaa huyo anadaiwa kuwa kwenye mipango kabambe ya kununua kituo cha runinga kinachomilikwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama cha Dira TV.Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Harmonize au Harmo, kwa sasa ni bampa to bampa kati ya jamaa huyo na aliyekuwa bosi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.Inaelezwa kuwa, Harmo anapitia hatua zote za Diamond au Mondi kwa kununua TV kama alivyofanya Mondi kwa kumiliki Wasafi TV.

“Hivi mnajua kuwa Harmonize naye anajipanga kuichukua Dira TV ya Msama?

“Harmonize na Msama wapo kwenye mazungumzo ya awali na hivi karibuni mtaona.(Jamaa (Harmo) amepania ile mbaya kuweka mguu alipoweka bosi wake na kwa hili la TV amedhamiria kushindana naye,” alisema mtu huyo.Mtu huyo aliongeza kuwa, mpaka sasa wafanyakazi wameshafahamishwa kuwa kutakuwa na bosi mpya ambaye ataingia na kwa waliomuona Harmonize akiwa karibu na Msama waliunganisha matukio.Baada ya habari hii kutua kwenye Dawati la Gazeti la Ijumaa Wikienda, waandishi walitinga kwenye ofisi za Dira TV maeneo ya Kinondoni jijini Dar ambapo walifanya uchunguzi wao na kubaini kuwepo kwa maneno hayo ndipo wakamsaka moja kwa moja mmiliki wa Dira TV ambaye alifunguka.Msama alipotafutwa alimwambia mwandishi kuwa hawezi kusema ni kweli au hapana isipokuwa ataita waandishi wakati utakapofika na ataweka wazi kila kitu.“Ninyi waandishi mnataka nini? Hizo habari siwezi kusema ni kweli au hapana ila muda utakapowadia nitaita waandishi nitawaeleza kila kitu,” alisema Msama aliyekuwa msimamizi wa matamasha makubwa ya Krismasi na Pasaka ambayo hivi karibuni alidai yamefungiwa.Baada ya kumsikia Msama, waandishi walimsaka Harmonize ili kuzungumzia jambo hilo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa na hata meneja wake, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ aliposakwa kuzungumzia hilo hakupatikana.

Gazeti hili linaahidi iwapo atapatikana tutaweka wazi ukweli wote.