Benki ya CRDB na Manispaa ya Wilaya ya Kigamboni leo zimeingia mkataba wa makubaliano wa mikopo ya uwezeshaji kwa wajasiriamali wamachinga na katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya Kigamboni, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Benki ya CRDB ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji mikopo hiyo ijulikanayo kama ‘Machinga Loans’.

“Mikopo hii imegawanyika katika sehemu mbili, kwanza tutakuwa na mikopo kwa mjasiriamali mmachinga mmoja mmoja, lakini pia tutakuwa na mikopo kwa wajasiriamli hawa waliopo kwenye vikundi,” alisema Nsekela.

Nsekela alisema uanzishwaji wa mikopo hiyo unatokana na juhudi za Serikali katika kuwarasimisha wajasiriamali wamachinga zilizofanyawa na Rais wa awamu ya tano Dokta John Magufuli mwishoni mwaka jana 2018 ambapo vitambulisho 1,850,000 vimetolewa.

“Vitambulisho vya wajasiriamali wadogo maarufu kama wamachinga vilivyotolewa na Mheshimiwa Raisi Magufuli, vimesaidia kuwarasimisha na hivyo kusaidia sana zoezi la utambuzi, hili ni jambo la muhimu sana ili kuwafanya wawe wanakopeshaka. Kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Raisi Magufuli na Serikali nzima ya awamu ya tano kwa kuendelee kutengeneza mazingira rafiki ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kiuchumi.

Nikupongeze pia Mheshimiwia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni kwa mikakati mizuri mnayoifanya ya uwezeshaji wajasiriamali katika Wilaya hii. Tukiwa Benki ya kizalendo tumevutiwa sana juhudi zenu na ndio maana tumeanza na mpango huu wa uwezeshaji wajasiriamali katika wilaya hii,” alisema Nsekela. Akiongelea namna ya utoaji mikopo hiyo, Nsekela alisema Benki ya CRDB inatumia mfumo wa kidijitali, kupitia huduma yake ya SIMAccount, ambapo mteja atawasilisha maombi ya mkoo kupitia simu yake ya mkononi na kupata mkopo wake ndani ya saa 24.

“Tumefanya hivi ili kuwaondolea wateja mlolongo mrefu wa kupata mkopo, hasa ukizingatia muda mwingi wanautumia katika sehemu zao za biashara,” aliongeza Nsekela.

Nsekela alisema katika utekelezaji wa mpango huo wa uwezeshaji ambao pi utahusisha elimu juu ya masuala ya fedha, uwekezaji, Bima na mikopo, Benki ya CRDB imeanza kwa kuwaunganisha wajasiriamali wamamchinga na huduma ya SimAccount ambapo mpaka sasa wajasiriamali 3,000 katika wilaya ya Kigamboni pekee wameshaunganishwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa Benki ya kwanza nchini kuitikia wito uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa kuwawezesha wajasirimali wadogo maarafu kama wamachinga.

“Hii ni fursa ya kipekee sana si tu katika wilaya yetu ya Kigamboni bali kwa Taifa letu kwa ujumla, ni imani yangu wajasiriamali wengi watakwenda kunufaika na mikopo hii pale itakapo sambaa katika wilaya zote nchi nzima,” aliongezea Sara Msafiri.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni alitumia fursa hiyo pia kuwasihi wajasiriamali wamachinga wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kujiunga na SimAccount ya Benki ya CRDB ili waweze kunufaika na mikopo hiyo pale itakapoanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) akibadilishana mikataba ya makubaliano wa mikopo ya uwezeshaji kwa wajasiriamali wamachinga na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Ng'ilabuzu Ludigija, huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sarah Msafiri (katikati) katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es salaam Septemba 17, 2019.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Ng'ilabuzu Ludigija wakisaini mkataba wa makubaliano wa mikopo ya uwezeshaji kwa wajasiriamali wamachinga wa Kigamboni, huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sarah Msafiri (katikati). Kushoto ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Ester Mwambapa na kulia ni Mwanasheria wa Manispaa ya Kigamboni, Charles Lawisso.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini baina ya Manispaa ya Kiganmboni na Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es salaam Septemba 17, 2019. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini baina ya Benki yake na Manispaa ya Kiganmboni, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es salaam Septemba 17, 2019. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri na kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Ng'ilabuzu Ludigija.