Waziri Ummy Akabidhi Mashine ya Upuliziaji Dawaza Kudhibiti Wadudu
Jiji la Tanga limekua la pili kupata mashine za kupulizia dawa za kuua mbu na wadudu wadhurifu waenezao magonjwa mbalimbali ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI katika kudhibiti wadudu hao.

Akikabidhi mashine hiyo kwa uongozi wa Jiji la Tanga, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mkakati huo ni wa miaka mitano (2019-2024) na unalenga kuhakikisha mbu na wadudu wadhurifu wanadhibitiwa kwa njia ya utengamano na ameiomba jamii ishiriki kikamilifu katika kupambana na wadudu hao.

"Wizara yangu imeagiza mashine nane za kisasa (foggig mashine) zenye uwezo mkubwa wa kupulizia na zinabebwa na magari na kupuliza eneo kubwa kwa wakati mmoja, hivyo naomba jamii ihakikishe inashiriki kikamilifu katika kupambana na wadudu hawa dhurifu,” Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa ni vema mikoa ikawekeza katika maeneo ya msingi am bayo ni pamoja na ushiriki wa jamii, sekta binafsi na wadau kushiriki katika kudhibiti wadudu kwa njia shirikishi zinazolenga kuharibu mazalia ya wadudu. Mikoa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa mbu na wadudu wadhurifu katika ngazi zote na kupanga njia madhubuti za udhibiti wa wadudu hao.

Waziri Ummy amesema katika kuhakikisha mkakati huu unatekelezwa, Wizara ya afya kwa kushirikiana na TAMISEMI imetoa maagizo kwa kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote ziweze kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ya utekelezaji wa udhibiti wa mbu na wadudu wadhurifu ambayo itakua mtaa kwa mtaa, Halmashauri kuhakikisha zinaishirikisha jamii katika ngazi zote za mapambano haya ya mbu na wadudu wadhurifu.

Pia Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kufanya tathmini ya utekelezaji wa mkakati huu katika kipindi cha mwaka mmoja na kutoa taarifa ya mafanikio, changamoto na mipango ya Halmashauri katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na kununua mashine za upuliziaji (Fogging Machine) angalau moja katika kipindi cha kufikia Januari 2020.