Waziri Mkuu Majaliwa Majaliwa amesema malengo ya Tanzania katika mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD7) ni kuishawishi Japan kuiunga mkono Tanzania katika suala la teknolojia na maendeleo ya viwanda ili kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya uchumi wa kati na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wake ifikapo 2025.

Majaliwa ameyasema hayo baada ya kuwasili katika Mji wa Yokohama Nchini Japan akimwakilisha Rais Magufuli kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD 7).

Akizungumza kabla ya kumpokea Waziri Mkuu, Waziri Prof. Kabudi amesema mkutano huo ambao unazikutanisha nchi za Kiafrika zinazoshirikiana na Japan katika suala la maendeleo utasaidia kutoa msimamo wa pamoja kuhusu maeneo ya vipaumbele kwa bara la Afrika ili kuleta maendeleo endelevu kupitia kauli mbiu ya Mkutano huo yA Kuendeleza Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi.