Waliosababisha Ndege Kukamatwa Sauz Kushitakiwa

MSEMAJI Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbas amesema watakaobainika walifanya hujuma dhidi ya  serikali  na kusababisha kuzuiwa kwa ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) nchini Afrika Kusini watafunguliwa kesi ya kuihujumu nchi baada ya kumalizika kwa kesi ya kuzuiwa kwa ndege katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini.Akizungumza mjini Dodoma leo Jumamosi Agosti 31, 2019,  Dkt.  Abbas amesema wapo Watanzania wanaoshiriki kuihujumu serikali  kuhusu ndege hiyo, wakifikiri kwamba kuna siku uhujumu huo utawasaidia.“Wapo wazawa wanaofanya mawili, matatu kuhujumu nchi lakini niwaeleze tusubiri kesi iishe huko Afrika Kusini, tutawafungulia kesi ya kuhujumu nchi yetu.“Hakuna nabii katika historia ya manabii aliyewahi kuaminiwa kwa asilimia 100, hivyo huwezi kukubaliwa na watu wote, hata hii ndege inayoshikiliwa ikija Tanzania ipo siku wanaochukia watatumia usafiri huo kwenda Afrika Kusini kama sio wao basi watoto wao,” amesema.