Wakazi wa Mtwara watakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao
Wakazi wa mkoa wa Mtwara wametakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili waweze kutumia vizuri fursa za ujenzi wa miundombinu ya barabara, anga na bandari kujiimarisha kiuchumi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi),Elius John Kwandikwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha ukanda wa kusini mwa Tanzania unafunguka kimiundombinu katika nyanja za barabara za lami, bandari na usafiri wa anga hivyo kazi inayowakabili wananchi ni kuongeza uzalishaji.

Akizungumza na wanakijiji wa Nanguruwe mkoani humo, Kwandikwa amesisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuweka fursa ya miundombinu bora katika kila kanda ili wananchi waitumie kukuza uchumi binafsi na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

“Tumejipanga kuhakikisha nyanja zote za usafiri zinaimarika katika ukanda huu wa kusini hivyo nawaomba zalisheni kwa wingi mazao ya chakula na biashara ili kufikia soko kwa haraka popote lilipo,” amesema Kwandikwa.

Aidha amemhakikishia mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha wilaya zote za mkoa wa Mtwara zinaunganishwa kwa barabara za lami katika kipindi kifupi ili kufikika kwa urahisi wakati wote na hivyo kuimarisha huduma za biashara.

Kwandikwa yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mtwara- Mnivata km 50 na uwanja wa ndege wa Mtwara unaorefushwa kutoka mita 2258 hadi mita 2800 hali itakayowezesha ndege nyingi na zinazochukua abiria wengi kutumia uwanja huo.