Na Woinde Shizza Michuzi Tv,Arusha

KIWANDA cha kusindika nyama cha Happy Sausage cha jijini Arusha kimeiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wao na Halmashauri ya Jiji la Arusha unaokwamisha kukuwa kwa uzalishaji na hivyo kushindwa kufikia soko la kimataifa ikiwemo la Afrika Mashariki.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho kiwandani hapo Andrew Goerge wakati akizungumza na vyombo vya habari kiwandani hapo kuelezea shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho pamoja na changamoto zao.

Amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha imeendelea kukwamisha juhudi za ukarabati wa kiwanda chao kwa kukataa kutoa kibali cha ukarabati wa (Bulding Permit) wakati Serikali kupia Wizara ya Mifugo na bodi ya nyama wameshatoa maelekezo ya kufanyika kwa ukarabati .

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa hatua hiyo imetokana na mgogoro wa muda mrefu unaofikia miaka nane kati ya pande hizo kuhusiana na suala zima la umiliki wa Ardhi wa eneo ambalo hadi sasa kila upande unavutia kwake wakati halmshauri hiyo ni mbia kati ya wabia 12 wa uwekezaji wa eneo la kiwanda .

“Kiwanda kimeshindwa kufikia malengo ya uzalishaji inatokana na kujikuta ikikwamishwa kufanya ukarabati wa kiwanda hicho cha usindikaji wa nyama kwa hali hiyo ambayo serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikikitaka kiwanda hicho kufanya ukarabati imekuwa ndio changamoto yetu kufikia malengo ya uzalishaji,"amesema George.

Amesema kuwa kiwanda hicho licha ya misukosuko hiyo katika kipindi cha miaka sita kimeweza kulipa wafugaji wanaokuja kuuza mazao ya mifugo kiasi cha Sh.bilion 9.3 na kuweza kilipa kodi ya Serikali leseni tozo na vibali mbali kiasi cha Sh.bilion 2.2 katika kipindi cha miaka sita.

Alieleza kuwa masoko yao makubwa ya kuuza bidhaa wanazozalisha ni masoko ya ndani ya nchi katika mikoa yote nchi kupitia mahoteli mbali mbali ya kitalii na maduka ya rejereja ya nyama nchini ambapo mpango wa kwa sasa ni kuelekea kwenye masoko ya nje ya nchi yakiwamo ya Afrika ya mashariki pamoja na Soko la pamoja la jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC.

Amesema kuwa kuhusiana na uzalishaji wa kiwanda hicho unavyobeba wananchi wengi wenye kuzalisha mazao ya mifugo kwenye kanda ya kaskazini na nchini kwa ujumla unaweza kuzorota kutokana na wao kushindwa kuleta mashine mpya .

Amesema kuwa kiwanda hicho wawekezaji wapo 12 akiwemo Halmashauri ya Jiji la Arusha ,ambao uwekezaji wake ulitokana na ardhi na kuridhiwa na baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Arusha wakati huo kwenye miaka ya 1990 ambacho kiwanda hicho kimejengwa ndani ya ardhi hiyo.

Ameeleza hapo awali kiwanda hicho kimekuwa kikifanyakazi na kiwanda cha Nyama cha Arusha Meat ambacho kwa sasa kinamilikiwa na halmashauri ya jiji la Arusha kwani hapo awali manispaa ilikuwa mbia kwa asilimia 49 wa kiwanda hicho ikiwa na asilimia 51

Amesema hatua ya mgogoro huo imesababisha kushindwa kufikia malengo ya uzalishaji pamoja mabenki kukataa kuwapatia mkopo , hivyo ameiomba Serikali kuingilia kati ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Mkurugenzi wake Dk. Maulidi Madeni kwa nyakati tofauti amekuwa akidai kiwanda hicho ni mali ya halmashauri hiyo na wanaojiita wamiliki wanania ya kutaka kukitaifisha .

Dk.Madeni amedai kuwa kwa muda mrefu amekuwa akimwita ofisini kwake mwenyekiti wa bodi ya Happy Sausage, Andrew George lakini ameshindwa kufika jambo ambalo ,George amedai si kweli kwa kuwa hakuwahi kuitwa na mkurugenzi huyo kwa mfumo rasmi wa kiofisi.