Baraza la Taifa la Sanaa (Basata) limesema wimbo Tetema wa msanii Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny aliomshirikisha Diamond Platnumz hauna tatizo lolote licha ya kuzuiwa kupigwa katika maeneo ya wazi nchini Kenya.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 27, 2019 na katibu mtendaji wa baraza hilo, Godfrey Mngereza alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kupigwa marufuku kwa wimbo huo Kenya.
Mngereza amesema hauna shida na hajui Kenya wametumia vigezo vipi kuuzuia.

“Tumekuwa tukifuatilia nyimbo za wasanii wa hapa nchini na kuwaita wanapokosea. Tunatoa onyo na hata kufungia nyimbo zao, lakini huu (Tetema) hauna shida ndio maana nasema sijui wametumia vigezo gani kuuzuia usichezwe mchana,” amesema Mngereza.

Wimbo huo pamoja na Wamlabez wa msanii Sailors wa nchini Kenya zimezuiwa kupigwa maeneo ya wazi na badala yake zinatakiwa kupigwa katika kumbi za starehe na baa