Ud Songo Wamfanyia Kitu Mbaya Chama
KIUNGO wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama, Jumamosi iliyopita ilikumbana na balaa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo uliofanyika nchini Msumbiji.Katika mchezo huo, Chama anadaiwa kupewa ulinzi mkali na wapinzani ili kuhakikisha hapati nafasi ya kuanzisha mashambulizi kama ambavyo alikuwa akifanya katika michuano hiyo msimu uliopita.Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa, kama Chama katika mchezo huo angekuwa sawa basi wangepata ushindi.“Tunamshukuru Mungu tumerudi salama japokuwa hatukupata ushindi lakini kazi ilifanyika, pia wapinzani wetu walijitahidi sana kuzijua mbinu zetu ambazo tumekuwa tukizitumia kupata ushindi.“Katika mchezo huo Chama hakufanikiwa kufanya vizuri kutokana na ulinzi mkubwa aliokuwa amewekewa na wapinzani wetu hao, kwani kila alivyokuwa akishika mpira tayari kuna watu wawili wanamzunguka jambo ambalo lilisababisha asifanye vizuri kama tulivyotarajia.“Hata hivyo ni matumaini yetu ni kuwa kocha atakuwa ameliona hilo na atalifanyia kazi ili katika mchezo wa marudiano tutakaocheza hapa nchini tuweze kupata ushindi,” alisema mchezaji huyo.Alipoulizwa Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems alisema: “Mchezo huo ulikuwa wa wazi na tulikuwa tukishambuliana kwa zamu na zaidi wapinzani wetu walijitahidi sana kuhakikisha wanadhibiti sehemu yetu ya kiungo ili viungo wetu wasipate nafasi ya kutengeneza nafasi za kufunga, hata hivyo katika mchezo wa marudiano tutahakikisha tunafanya vizuri katika uwanja wetu wa nyumbani.”