Rais wa Marekani, Donald Trump amekanusha taarifa ya kwamba alimwambia mkuu wa chama kinacholinda haki ya raia kumiliki bunduki nchini humo-NRA kwamba kuongeza historia ya uchunguzi kwa wanunuzi wa bunduki sio moja ya masuala ya kujadiliwa.

Trump amesema kuwa anaunga mkono hatua hiyo ya kuongeza uchunguzi kwa wanunuaji wa bunduki kwani matukio ya mauaji yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ikulu ya nchi hiyo, ‘White House’ siku ya Jumatano wakati akielezea namna anavyopanga kukabiliana na ghasia za bunduki nchini Marekani.

Aidha, amesema kuwa bado anafikiria njia za kuboresha zaidi uchunguzi kwa wanunuaji wa bunduki lakini alionya kile anachoita kuwa wazo ambalo kwa kiasi fulani haliendani na kipengele cha pili cha katiba ya Marekani.

Trump ameongeza kuwa anataka bunduki kuwa mikononi mwa watu ambao hawana matatizo ya akili na anataka watu hao waweze kupata bunduki kiurahisi.