Kisiwa cha Greenland kimesema kwamba hakiuzwi baada ya rais Donald Trump wa Marekani kusema kwamba angependa Marekani kukinunua kisiwa hicho kikubwa duniani.

Rais huyo alidaiwa kuzungumzia wazo hilo la kukinunua kisiwa hicho cha Greenland - eneo la Denmark linalojitawala katika chakula cha jioni na mikutano na washauri wake.

Lakini Serikali ya Greenland imepinga wazo lake ikisema kwamba wako tayari kwa biashara lakini sio kununuliwa.


Mipango ya rais Trump pia imepingwa na wanasiasa wa Denmark.

''Inaonekana ni mzaha wa siku ya wajinga ya Aprili mosi'', alituma ujumbe wa twitter waziri mkuu Lars Lokke Rasmussen.

Jarida la wall Street Journal lililochapisha habari hizo lilisema kwamba bwana Trump alizungumzia kuhusu ununuzi huo.

Duru zilizonukuliwa na vyombo vingine vya habari zilitofautiana kuhusu iwapo rais huyo alikuwa akifanya mzaha huku akiwa na wazo la kupanua himaya ya Marekani.

Maafisa katika kisiwa hicho cha Greenland wamesisitiza kwamba kisiwa hicho hakiko katika soko.

''Greenland ina utajiri wa madini, maji safi zaidi na barafu, samaki, chakula cha baharini kawi na ni kivutio kikuu cha utalii. Tuko wazi kwa biashara lakini sio kuuzwa'', ilisema wizara ya kigeni katika taarifa yake iliotumwa katika mitandao ya kijamii.

Waziri mkuu wa Greenland Kim Kielsen alirejelea matamshi yake katika taarifa nyengine tofauti .

''Greenland haiuzwi lakini iko wazi kibiashara na ushirikiano na mataifa mengine'', ilisema taarifa.

Mbunge wa Greenland Aaja Chemnitz Larsen pia alikuwa miongoni mwa wale waliopinga hamu hiyo ya rais wa Marekani.

''Hapana ahsante kwa bwana Trump kununua Greenland'' , aliandika katika mtandao wa Twitter, akiongezea ''ushirikiano wa usawa kati ya Marekani na Greenland ndio suluhu pekee''.

Poul Krarup muhariri mkuu wa gazeti la Sermitsiaq aliambia BBC hakuamini matamshi ya bwana Trump. ''Greenland ni sehemu ilio huru katika ufalme wa Denmark na inahitaji kuheshimiwa'', alisema.

Lakini alisema kwamba alidhani kwamba ndoto ya Bwana Trump haiwezi kuafikiwa.

''Tungependa kushirikiana na Marekani , bila shaka lakini sisi tuko huru na tunaamua marafiki zetu ni akina nani''.