Tatuu ya Mondi kwa Mobeto Yazua Gumzo
SIRI imefichuka kwamba, kumbe modo ambaye ni mwigizaji na msanii wa Bongo Fleva, Hamisa Mobeto ‘Misa’ amejichora tatuu ya baba wa mtoto wake, Dyllan Nasibu, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na kuibua gumzo kama lote.  Wikiendi iliyopita zilisambaa picha zilizomuonesha Mobeto akiwa na tatuu hiyo ya Diamond au Mondi aliyojichora mgongoni chini ya kwapa la mkono wa kushoto.

Tatuu hiyo ni ya jina la Chibu ambalo inasemekana Mobeto hupendelea kumwita jina hilo Diamond. Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Mobeto, tatuu hiyo alijichora kipindi kile alipokuwa kwenye mapenzi mazito na jamaa huyo, lakini sasa imekuwa ikimpa taabu sana.

“Ndiyo maana Misa (Mobeto) amekuwa mgumu sana kuingia kwenye uhusiano na mwanaume mwingine maana tayari ana alama hiyo ya Mondi ambayo haifutiki kirahisi. “Hivi itakuwaje akipata mwanaume mwingine halafu akawa anaiona hiyo tatuu ya Mondi? Hapa pana funzo kubwa sana, yaani unajichora tatuu ya mtu halafu mkiachana inakuwaje?” Ndivyo zilivyosomeka baadhi ya ‘komenti’ kuhusu ishu hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Alipotafutwa Mobeto kufungukia ishu hiyo simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu hivyo jitahada zinaendelea. Mobeto alidaiwa kuchepuka na Mondi wakati jamaa huyo akiwa kwenye uhusiano na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambapo walifanikiwa kupata mtoto huyo mmoja wa kiume ambapo uhusiano wao pia uliishia hapo.