Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia mashabiki na wapenzi wa timu ya Soka ya Simba wakati alipoingia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwa mgeni rasmi katika Simba Day, Agosti 6, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Simba Day kwenye uwanja Taifa jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Kulia ni Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji na kushoto ni Rais wa TFF, Wallece Karia. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaridhishwa na maendeleo ya soka la Tanzania.
“Serikali inaridhishwa na maendeleo ya soka la Tanzania. Soka la Tanzania limeanza kukua kwa kiwango kizuri. Timu za Tanzania zinashiriki mashindano ya kimataifa na sasa hivi zinashinda. Tumeona Taifa Stars imeishinda timu ya Kenya, nayo timu ya Taifa ya wanawake imeishinda timu ya Swaziland,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumanne, Agosti 6, 2019) wakati akizungumza na mashabiki wa timu ya Simba Sports Club mara baada ya kukagua timu hiyo na Power Dynamos ya Zambia kabla ya kuanza kwa mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Simba Day, amesema mafanikio yanayopatikana hivi sasa kwa ushindi wa timu za Tanzania ni matokeo ya kuwa na vilabu imara vya soka kama vile Yanga, Simba, Azam au Namungo.
“Nyote ni mashahidi kuwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuwa anataka kuona Tanzania inashinda makombe ya Afrika, na hii ni fursa kwa timu ya Simba kuonesha hilo kupitia mechi hii ya leo.”
“Leo tunashuhudia mechi kati ya Simba Sports Club na Power Dynamos ya Zambia na uwanja umejaa, umefurika. Ninaiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, isimamie vilabu vyote ili viwe na mifumo mizuri ya mapato,” amesema.
Amewataka Watanzania waendelee kuisapoti timu ya Taifa kila inaposhiriki mashindano ya kimataifa. “Natambua kuwa mwezi ujao, timu yetu itacheza na Burundi na Sudan. Kwa hiyo ninawasihi Watanzania kuishamgilia timu yetu kama tulivyojaa leo,” amesema.
Mapema, kabla ya mchezo huo kuanza, timu ya Simba iliamua kuwatambulisha wachezaji wake ambao imewasajili katika msimu huu pamoja na benchi lake la ufundi.
Wachezaji waliotambulishwa leo ni Rashid Juma, Ally Salim, Yusuph Mlipili, Mzamiru Yassin, Kennedy Juma, Mohammed Hussein, Jonas Mkude, Miraji Othman, Haruna Shamte, Hassan Dilunga, Shomari Kapombe, Aishi Manula na Pascal Wawa.
Wengine ni Henrique Wilker, Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga, Beno Kakolanya, Deogracias Kanda, Clatous Chama, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Meddie Kagere, Sharaf Shaibob, Francis Kahata, John Bocco na Ibrahim Ajib.
Waliotambulishwa kwenye benchi la ufundi ni kocha wa timu hiyo Patrick Aussems, kocha msaidizi Dennis Katambi, Adel Zbane, Yassin Gembe, Abbas Ally, Hamisi Mtambo, Patrick Rweyemamu (Meneja) na Muharam Mohammed.