Washiriki wa mafunzo ya kupinga mila potofu ya ukeketaji wakionesha mshikamano wa mapambano dhidi ya vitendo hivyo baada ya kuunda kamati za ulinzi wa mama na mtoto katika Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida juzi.
 Mwezeshaji wa mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu, Japhet Kalegeya  akizungumza katika mkutano wa kuunda kamati za ulinzi wa mama na mtoto wilayani Ikungi mkoani humo.
 Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ikungi, Haroon Haroon akiwasilisha mwongozo wa ( MTAKUWA) kwa kamati za ulinzi wa mama na mototo ngazi ya Kata sita za Ikungi,Ihanja, Iglanson, Iseke,  Mhintiri  na Minyughe.
 Mwezeshaji, Daniel Saido akiwa na Mratibu wa mradi huo, Evaline Lyimo katika mkutano huo.
Diwani wa Kata ya Ihanja, Sombi Majuta  akizungumza katika mkutano


 Wadau mbalimbali wakiwa katika mkutano huo.
Mratibu wa mradi huo, Evaline Lyimo akizungumza katika mkutano huo.Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA la Foundation for Civil Society (FCS) limetoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya mradi wa kupambana na mila potofu za ukeketaji mkoani Singida ambao umeanza mwezi Julai hadi Machi 2020. 

Fedha hizo zimetolewa kwa Shirika lisilo la kiserikali la Save the Mother and the Children of Central Tanzania (SMCCT), ambalo limeunda kamati za ulinzi wa mama na mtoto kwenye kata sita na vijiji 18 katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa ajili ya mapambano hayo. 

Imeelezwa kwamba majukumu ya kamati hizo ni kumlinda mama na mtoto dhidi ya vitendo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia. 

Hayo yalisemwa na mwezeshaji wa mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu, Japhet Kalegeya wilaya ni hapa juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo ambao utasaidi kupunguza vitendo hivyo au kuvimaliza kabisa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali. 

Alisema wamefikia uamuzi wa kuanzisha kamati hizo ili ziweze kuharakisha kutokomeza kabisa vitendo hivyo ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu kama vile ukatili dhidi ya wanawake na watoto, mimba za utotoni, ndoa za utotoni ,ubakaji ,ulawiti,ukeketaji na udhalilishaji wa kijinsia katika  wilaya hiyo. 

“Mradi huu wa utetezi dhidi ya mila potofu ikiwemo ukeketaji na ukatili wa kijinsia unalenga kuwafikia wanawake na wasichana wapatao 7,200 katika wilaya ya Ikungi ambapo hali ya  unyanyasaji wa kijinsia ni mbaya”, alisema Kalegeya.

 Akitolea mfano wa hali hiyo alisema  kuanzia Januari hadi oktoba 2018 jumla ya wanafunzi 23 waliokuwa kati ya kidato cha kwanza na nne walipachikwa mimba wilayani Ikungi.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Sekondari ya Masinda, Rosemary Seith, amelishukru na kulipongeza shirika la SMCCT kwa kushirikisha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwapa elimu juu ya madhara ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia. 

“Sisi tuliohudhuria mafunzo haya yametusaidia kujua kwa mapana madhara ya vitendo hivyo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia sasa tunaenda kuwaelimisha na wenzetu ambao hawakubahatika kupata mafunzo haya hapa leo”, alisema. 

Mratibu wa mradi huo, Evaline Lyimo, ametaja baadhi ya malengo ya mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa uelewa kwa jamii kuhusu kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji na kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii hadi ifikapo Machi mwaka 2021.

Kata zilizounda kamati hizo ni lkungi, Ihanja, Iglansoni,Iseke, Minyughe na Muhintiri.