Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amelitaka Shirikisho la Michezo kwa shule za Sekondari za Afrika Mashariki (FEASSSA) kuwa na mipango ya pamoja ya kuendeleza vipaji vya watoto vinavyoibuliwa kupitia mashindano ya FEASSSA.
Akifungua mashindano hayo leo kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mhe.Jafo amesema lazima viongozi wa michezo kutoka nchi wanachama za Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa wabnakwenda kuvilea vipaji vya wanamichezo vitakavyopatikana kupitia mashindano hayo.
Amesema kuna tabia imejengeka kwamba watoto wenye vipaji wanaibuliwa kupitia michezo hiyo lakini vipaji hivyo vinapotea kwa kukosa matunzo na hivyo kupotea.
“Niwaombe nchi wanachama kila mmoja katika nchi anayotoka twende tukavilee vipaji mbalimbali vitakavyoibuliwa kupitia mashindano hayo,” amesema na kuongeza:
“Ninaamini tukifanya hivyo tutatenda haki sawa na changamoto kubwa ipo kwa wasichana ambapo taarifa zinaonyesha kuwa vijana wengi mahiri wasichana licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kimichezo lakini mdondoko umekuwa ni mkubwa.”
Mhe.Jafo amewataka waratibu wa nchi mbalimbali zinazoshiriki michezo hiyo kwenda kuwalea vijana wenye vipaji ili kuweza kuendeleza vipaji vya vijana hao kwa maendeleo ya michezo katika nchi zao.