Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amepiga marufuku watumishi wa Serikali kwenda likizo kwa muda wa miezi mitatu, ili kusimamia miradi ya Maendeleo na vitambulisho vya wajasiriamali kwenye maeneo yao, na maandalizi ya mapokezi na uzimaji wa Mwenge wa Uhuru.

Ameweka zuio hilo alipokuwa anazungumza katika kikao kazi na watumishi mbalimbali, wakiwemo Ma Ofisa Tarafa na watendaji Kata wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa ya Lindi kilichofanyika uwanja wa Ilulu mjini humo.

Amesema kuwa amechukua uamuzi huo kufuatia Shughuli nyingi inazoukabiri Mkoa huo kwa mwaka huu, kama vile uzimaji mwenge wa Uhuru utakaohitimisha mbio zake na kumbukizi za kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere Oktoba 14 mwaka huu na haraiki ya vijana.

Aidha, amesema kuwa kutokana na majukumu hayo, amelazimika kuzuia watumishi wote wa Serikali, Wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa, Ma-Ofisa Tarafa, watendaji Kata, vijiji, Mitaa na vitongoji kutoenda likizo, kwa muda hadi pale zitakapokamilika shughuli hizo.

Zambi amezitaja sababu nne, ikiwemo ujio wa Mwenge wa Uhuru, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, shughuli za vijana na ukamilishaji wa zoezi la uuzwaji wa vitambulisho vya wajasiriamali.


“Kuanzia leo nazuia likizo zote za watumishi wote wa Serikali hadi mwezi Disemba mwaka huu,”amesema Zambi.


Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Mkoa una miradi mingi, kama vile ujenzi wa vituo vya Afya, Zahanati na Shule lakini kutokana na kukosa usimamizi wa karibu imekuwa ikilegalega utekelezaji wake.