Rais wa kwanza wa Gambia na mwasisi wa uhuru wa nchi hiyo, Dawda Jawara, amefariki dunia Jumanne, Agosti 27 akiwa na umri wa miaka 95.

Familia yake imethibitisha kutokea kwa kifo chake na kusema kuwa kimetokea katika makazi yake huko Fajara, kilomita 15 kutoka mji mkuu Banjul.

Aidha, Dawda Jawara alikuwa rais mkongwe zaidi wakati alitimuliwa madarakani mnamo mwezi Julai 1994. Wakati huo alikuwa ametumia zaidi ya miaka 24 akiwa Rais wa Jamhuri ya Gambia.

Kabla ya hapo, Dawada Jawara, ambaye alizaliwa mwaka 1924, alisomea nchini Scotland, na alirudi nchini mwake mwanzoni mwa miaka ya 1950 kama daktari wa mifugo na alianza kujishughulisha na siasa mwaka 1960 baada ya kujiunga na Chama cha Progressive People.