Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa ametembelea kambi ya Mazimbu mkoni Morogoro eneo ambalo mamia ya wapigania uhuru toka Afrika Kusini waliishi na na kufanyia mafunzo wakati wa ubaguzi wa rangi.
Akishukuru Ramaphosa amalitaja eneo hilo kuwa Macca ya harakati za ukombozi wa Afrika kusini na kuwashukuru ndugui zao watanzania kwa msaada wao wa hali na mali katika kipindi hicho kigumu katika historia ya taifa lao
Eneo hilo lilitolewa kwa Afrika Kusini na muasisi wa Taifa la Tanzania hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere na sasa liko chini ya uangalizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine kilichopo mkoani Morogoro.
Ramaphosa amesema eneo hilo ni muhimu kwake binafsi kwani sehemu ya familia yake imeishi kwenye kambi hiyo kwa muda mrefu.
"Watoto wawili wa kaka yangu wamezaliwa hapa, hivyo eneo hili ni sehemu ya maisha yangu milele kwasababu vitovu vyao vilizikwa hapa," amesema Ramaphosa.
Ramaphosa pia aliembelea eneo la makaburi ambapo baadhi ya wapigania uhuru hao walizikwa: "eneo hili wamezikwa watu waliokuja kutoka Afrika Kusini na wengine walizaliwa hapa kwa ajili ya kupigania uhuru, tunawashukuru watu wa Morogoro kwa ushirikiano mliowapa walioishi hapa."
Pia ameiomba serikali ya Tanzania kufikiri namna ya kuliendeleza eneo hilo kuwa kivutio cha utalii kwa siku za usoni.
Ramaphosa yuko Tanzania kwa ajili mkutano wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Mendeleo ya Kusini mwa Afrika ambao utafanyika mwishoni mwa juma jijini Dar es salaam.
Tayari wakuu kadhaa wa mataifa hayo wameshawasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano huo.
Rais Mwenyeji John Magufuli wa Tanzania atachukua kijiti cha kuiongoza jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja toka kwa Mwenyekiti wa sasa Rais wa Namibia Hage Geingob.