Rais  Magufuli amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa kusimamia wawekezaji wasisumbuliwe katika uwekezaji wa viwanda.

Rais Magufuli pia amewaomba Watendaji ndani ya Serikali kutowasumbua wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza nchini.

Ametoa tamko hilo leo Alhamisi Agosti 1, alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kusaga Nafaka cha 21st Century Food and Packaging, kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, kinachomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo Dewji).

“Watendaji ndani ya serikali pamoja na Waziri wa vianda yuko hapa, tusiwaumize vichwa wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza katika nchi yetu, nimepata taarifa kuna baadhi ya wawekezaji wanawekewa masharti ya ajabu na wengine wanaombwa rushwa, sasa mnawazungusha kwanini hela ni yake haujamsaidia yeye anakuja kuwekeza ili watu wako wapate ajira,” amesema

“Waziri wa Biasha kama kuna watendaji wako ndani ya serikali bado hawajaona mwelekeo wa awamu ya tano wakae pembeni sisi tuendelee kwenda mbele kwani tunataka wawekezaji waje, akiwa na hela yake muoneshe eneo akajenge kiwanda chake na akishamaliza serikali itakusanya kodi, Tanesco watauza umeme, Dawasco watauza maji kwani hiyo ndiyo njia ya kuijenga nchi,”

“Waziri wewe ni kijana nenda ukafanye kazi kwa manufaa ya nchi, na mimi ninawaomba mkatangaze mema ya nchi yetu kwani serukali ya Tanzania ya awamu ya tano inapenda wawekezaji ndio maana tumefuta kodi zaidi ya 54 na sio rahisi kufanya hivyo lakini tunafanya kwa kuangali mbele,” amesema.