Pambano la marudiano kati ya Andy Ruiz Jr na Anthony Joshua litafanyika mwezi Disemba nchini Saudi Arabia, promota wa Joshua Eddie Hearn amethibitisha.

Kumekuwa na tetesi kuwa Ruiz Jr hayupo tayari kwa pambano hilo, lakini Hearn amesema kuwa mabondia wote wawili wameshaini kucheza mpambano huo Disemba 7 mwaka huu.

Ruiz aliushangaza ulimwengu wa masumbwi kwa kumchakaza Joshua mwezi Juni na kutawazwa kuwa bingwa wa dunia.

Bingwa huyo mpaka sasa hajawaarifu chochote mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na mpambano huo wa marejeano toka ulipotangazwa siku ya Ijumaa.

Mkufunzi wake, Manny Robles amesema "kuna sababu inayommfanya" Ruiz kukaa kimya.


"Mabondia wote wawili wameshatia saini. Vyombo vya usimamizi (wa ndondi) vimeshaarifiwa," amesisitiza Hearn.

Katika mkutano na wanahabari, ambao hata hivyo si Joshua wala Ruiz ambaye alihudhuria, Hearn alitangaza kuwa mpambano huo utafanyika katika uwanja wa wazi katika kitongozji cha Diriyah, nje kidogo ya jiji la Riyadh.

Omar Khalil, ambaye anafanya kazi na Serikali ya Saudia katika kuandaa pambano hilo pia ametangaza kuwa wote watakaonunua tiketi za mpambano huo moja kwa moja watakuwa wamepewa viza ya kuingia nchini humo.

Upande wa Ruiz uliweka wazi kuwa usingekubali kucheza pambano la marejeano nchini Uingereza huku upande wa Joshua ukitaka pambano hilo lichezwe nje ya Marekani.

"Tulipata ofa kutoka Saudi Arabia, Abu Dhabi, Dubai na Qatar," aliongezea Hearn. "Tulitaka kwenda sehemu ambayo wana maono ya mbali na mchezo wa masumbi. Tulijua Saudia inamaanisha na imewkeza kwenye mchezo huu."

"Inabidi tutambue kuna ulimwengu mwengine nje ya Uwanja wa Cardiff na Madison Square Garden. Tunalazimika kukuza mchezo huu katika maeneo mengine duniani.